JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Viongozi wa Umma Waaswa Kuwa Waadilifu
27 Oct, 2023
Viongozi wa Umma Waaswa Kuwa Waadilifu

Viongozi wa Umma wametakiwa kuwa waadilifu katika utendaji kazi wao wa kila siku.Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi alipokua akifungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa Mkoa wa Mwanza yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Wakala wa Barabara (TANROADS) Kanda ya Ziwa - Mwanza tarehe 21 Septemba 2023.

Mhe. Makilagi alifafanua kuwa Maadili ni nguzo muhimu katika kufanikisha mipango na maelekezo ya nchi kwani usaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa rasilimali za umma pamoja na kudhibiti mianya ya rushwa.

Mhe, Makilagi katika hotuba yake aliongeza kuwa, Maadili yanajenga na kudumisha amani ya nchi kwani Viongozi wanapokua waadilifu wananchi wanakua na amani “Tumeona kwa wenzetu wananchi wanapokosa imani na Serikali yao amani inapotea kunatokea fujo, wanaandamana na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi na kuleta madhara mengi hivyo niwaase Viongozi wenzangu tusiifikishe Serikali na Taifa letu huko kwa jambo dogo tuu la kukosa Maadili” alisema.

Aidha Mhe Makilagi aliwasisitiza Viongozi hao kuwa waadilifu katika kusimamia na kutoa maamuzi ya haki “Unapokua na uadilifu usiokua na mashaka unakua na ujasiri wa kusimamia sheria na kutoa maamuzi kwani unachokisimamia ndicho unachokiishi ” alisema.

Mhe.Makilagi aliwaasa Viongozi hao kuhakikisha kuwa wanakua na uelewa wa kutosha kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kanuni za utumishi wa umma pamoja na suala zima la mgongano wa maslahi.

Katika hotuba yake Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa suala la Mgongano wa maslahi katika Utumishi wa Umma limekua changamoto kubwa sana kwa serikali kwani baadhi ya Viongozi na watendaji wasio waadilifu wamekua wakijiingiza katika mgongano wa maslahi kwa lengo la kujinufaisha wao binafasi na familia zao.

“Niwaombe mkitoka hapa suala la mgongano wa maslahi likaishe kabisa katika utendaji kazi wetu tukafanye kazi kwa maslahi ya watanzania wote kwani kunapokua na mgongano wa maslahi mahala popote kunachelewesha ama kudumaza kasi ya maendeleo ya ukuaji wa uchumi” alisema

Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha kuwa Viongozi na watumishi wa Umma kuwa waadilifu, waaminifu na wanafanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu hivyo mafunzo ya mara kwa mara yanahitajika kwa Viongozi na Watumishi hao.

Awali akitoa neno la utangulizi Katibu Msaidizi kanda ya Ziwa _Mwanza Bw, Godson Kweka alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi wa Umma kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuwakumbusha Viongozi kujiepusha na masuala yote yanayohusiana na mgongano wa maslahi, pia kuwakumbusha Viongozi wa Umma kuzingatia na kuishi kiapo cha Ahadi ya Uadilifu wanachoapa mara tuu ya kuteuliwa ama kuchaguliwa, pamoja na kuwakumbusha Viongozi kuzingatia uwajibikaji wa pamoja katika utendaji kazi wao.

“Tumesikia mara kadhaa kumekua na kutoelewana kati ya Viongozi kwa Viongozi mfano Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, Mkuu wa Taasisi na watendahi wengine ndio maana tumekuja kuwakumbusha kuwa migogoro ya namna hiyo haina afya kwa Serikali yetu kwani inaitia doa serikali na kukwamisha ama kuchelewesha maendeleo kwa wananchi” alisema.

Aidha Bw.Kweka alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili imekua ikipokea malalamiko mbalimbali yanayowahusu Viongozi wa Umma yanayohusiana na masuala ya ardhi, matumizi mabaya ya madaraka, uonevu unaofanywa na baadhi ya Viongozi na watumishi wa Umma, malalamiko kuhusu kutokutendewa haki, upendeleo, watumishi kutolipwa stahiki zao pamoja na mengine mengi.

“Viongozi tuyachukue malalamiko haya kama changamoto twende tukajikague katika utendaji kazi wetu twende tukatatue kero za wananchi ili tuweze kutoa huduma bora kwa wananchi” alisema.

Mafunzo hayo yalitolewa kwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mwanza, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala wa Wilaya, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza pamoja na Makamanda wa Polisi Wilaya ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Uwajibikaji wa pamoja na Mgongano wa Maslahi

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >