Viongozi wa Umma mkoani Kagera watakiwa kuepuka Mgongano wa Maslahi.

Katibu Tawala Msaidizi Rasilimaliwatu Mkoa wa Kagera Bw. Bwai Mashauli Biseko amewataka Viongozi wa Umma mkoani Kagera kuepuka vitendo vinavyoashiria uwepo wa mgongano wa masilahi ili kuweza kuwasimamia watumishi waliochini ya Idara zao na kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia weledi na maadili katika kutekeleza majukumu yao.
Bw. Biseko akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo kuhusu maadili ya Viongozi wa Umma yaliyofanyika mkoani Kagera katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba tarehe 8 Mei, 2025.
Bw. Biseko amebainisha kuwa swala la mgongano wa masilahi katika utumishi wa umma limekuwa likiathiri sana ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu ya Serikali ambapo baadhi ya Viongozi wasio waadilifu wamekuwa wakijiingiza kwenye mgongano wa masilahi kwa lengo la kujinufaisha wao ,familia zao,pamoja na marafiki zao.
”Jambo hili limekuwa likisababisha kasi ndogo ya ukuwaji wa uchumi pamoja na utoaji wa huduma duni kwa wananchi,” amesema.
Aidha Bw. Biseko amefafanua kuwa ili kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa ni vyema elimu kuhusu Sheria ya Maadili pamoja na mgongano wa Maslahi iwe inatolewa mara kwa mara kwa Viongozi wa Umma,Watumishi wa Umma pamoja na sekta binafsi.
Katika hatua nyingine Bw. Biseko amewataka washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Viongozi wa Umma kutumia vyema elimu waliyopata kupitia mafunzo hayo ili kuleta mabadiliko na hatimaye kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na nidhamu kwa maendeleo ya Taifa.
Awali akiongea na washiriki wa mafunzo hayo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Mhe. Godson Gupson amesema kuwa uwepo wa mgongano wa maslahi kwa Viongozi umekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu kwa Viongozi jambo linalopelekea uwepo wa maamuzi yasiyokubalika.
“Mgongano wa Maslahi unapunguza tija katika utendaji wetu na kusababisha Serikali kutotekeleza majukumu yake kwa kiwango kinachostahili na kupoteza ufanisi wa shughuli za Serikali,” amesema.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Bi.Fatina Laay ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba amesema mafunzo waliyopatiwa yatasaidia katika kukuza maadili kwa Viongozi waliyopo chini yao na kuhakikisha wanakua makini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yamewashirikisha Viongozi wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi mbalimbali pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi wengine wa Umma wakiwemo Mahakimu wa Mahakama za Wilaya.