Viongozi wa Umma mia sita hamsini na nane kuhakikiwa

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inatarajia kuanza zoezi la uhakiki wa Raslimali na madeni ya viongozi wa umma kuanzia tarehe 7 Novemba hadi tarehe 18 Novemba 2022.
Jumla ya Viongozi wa Umma mia sita hamsini na nae (658) wanatarajiwa kufanyiwa uhakiki wa rasilimali namadeni yao ambapo zoezi hilo litafanyika katika mikoa ya Dar es salaam ,Njombe, Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Geita, Mwanza, Tabora, Tanga .
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alipokua akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mapema wiki hii katika ukumbi wa Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jijini Dodoma.
Mhe. Kamishna katika taarifa yake alisema kuwa, pamoja na majukumu mengine yanayotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili , Sekretarietiya Maadili inalo jukumu kubwa la kufanya uhakiki wa matamko ya rasilimali na madeni ya Viongozi wa Umma. “Zoezi hili hufanyika kwa awamu na katika awamu hii tumechagua idadi hiyo ya viongozi kufanyiwa uhakiki wa rasilimali na madeni yao” alisema.
Aidha Mhe. Kamishna alitoa rai kwa Viongozi wote waliochaguliwa kufanyiwa uhakiki huo kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa timu zilizoteuliwa kufanya uhakiki katika maeneo yao pamoja na kufanya maandalizi kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa kupitia barua walizotumiwa ili kuweza kurahisisha zoezi hili.
Aidha, Mhe. Kamishna alihitimisha taarifa yake kwa kuwakumbusha Viongozi wa Umma kutoa matamko ya Rasilimali,Maslahi na Madeni ya mwaka 2022 kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,na kwamba mwisho wa kurejesha fomu hizo ni tarehe 31 Disemba, 2022. Aidha fomu hizo zinapatikana katika tovuti ya taasisi ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz.