Viongozi wa Manispaa ya Bukoba waaswa kuwa waadilifu

Viongozi wa Manispaa ya Bukoba wametakiwa kuwa waadilifu, waaminifu na kuepuka migongano ya maslahi katika utendaji kazi wao ili kulinda viapo vyao.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Dkt. Toba Nguvila alipofungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa umma wa Manispaa ya Bukoba yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera tarehe 25 Januari, 2024.
Dkt. Nguvila aliwaeleza Viongozi hao kuwa ipo haja ya kujenga na kulinda utamaduni wa kuzingatia maadili sahihi katika taasisi wanazotumikia na kusimamia maadili kwa katika Taasisi wanazoziongoza.
”Kama mnavyofahamu suala la maadili ni nguzo muhimu sana katika jamii kwani maadili yanasaidia kudhibiti mianya ya rushwa na vitendo vingine visivyo na Maadili na kuleta amani na utulivu katika jamii jambo linalotuwezesha kufanikisha mipango ya maendeleo katika nchi yoyote ile duniani hivyo, tunapaswa kulipa kipaumbele,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Dkt. Nguvila, suala la mgongano wa Maslahi kwa viongozi limekuwa likiathiri utendaji kazi kwa baadhi ya viongozi na kushauri elimu kuhusu Mgongano wa Maslahi itolewe kwa kiwango cha juu kabisa katika jamii yetu.
Aidha, Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Kagera amewataka Viongozi wa Umma kupitia mafunzo hayo kubadilika katika utendaji wa kazi na kuongeza nidhamu ya Maadili ili kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza pamoja na Serikali kwa ujumla.
Awali akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa- Mwanza Bw. Godson Kweka alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi wa Umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Alisema, Mafunzo hayo yalilenga kuwakumbusha Viongozi wa Umma kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwaingiza katika mgongano wa maslahi kwani tatizo hilo ni kubwa sana na linaathiri maendeleo ya nchi.
“Viongozi na watumishi wenzangu sisi kama Taasisi inayosimamia maadili tumekuja kuwakumbusha kuwa mnaposhughulikia miradi ya serikali msiingize masuala yenu binafsi mfanye maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya umma,” alisema.
Washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja walikuwa Kamati ya Usalama ya mkoa wa Kagera, Viongozi wa Mahakama, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo Sekretarieti ya Mkoa, Madiwani na Wakuu wa Idara na Vitengo Manispaa ya Bukoba.
Mada zilizowasilishwa ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Uwajibikaji wa pamoja, pamoja na Mgongano wa Maslahi.