VIONGOZI SITA WAFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA MAADILI:

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewafikisha mbele ya Baraza la Maadili Viongozi sita wa Umma kwa kushindwa kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili kinyume cha Sheria.
Viongozi waliofikishwa mbele ya Baraza la Maadili tarehe 27 Machi, 2025 katika ukumbi wa ofisi za Sekretarieti ya Maadili ni; Mhe. Edward Mhina Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba wa wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Mhe. Mwandei Mohamed, diwani halmashauri ya wilaya Mkinga, Mhe. Mussa Bohero Jangwa diwani wa kata ya Mayomboni, Tanga na Bi. Mwajuma Abas Kihiyo, Msajili wa Hati Msaidizi, Tanga.
Viongozi wengine ni Bw. Idefonce Columba, Meneja wa TANESCO wa wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, Mhe. Cleopha Mziray, hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Puge, mkoani Tabora.
Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Emma Gelani ameliambia Baraza kuwa walalamikiwa wote sita kwa pamoja wanadaiwa kushindwa kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili kinyume na misingi ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Sura ya 398.
“Mhe. Mwenyekiti, kushindwa kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni ni ukiukwaji wa misingi ya uongozi kwa mujibu wa kifungu cha 9(1)(b) na kifungu cha 16(a) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema.
Viongozi hao wanatuhumiwa kushindwa kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kati ya mwaka 2021 hadi 2023.
Walalamikiwa wote katika nyakati tofauti wamekiri kosa.
Mmoja wa watuhumiwa hao Bw. Musa Jangwa alipoulizwa na Mhe. Rose Teemba, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili kama amesikia malalamiko yake amesema, “Ndio nimeyasikia Mhe. Nakiri kosa na naliomba Baraza lako linisamehe aksante.”
“Kwa kuwa maelezo yametolewa na umekiri kwa kinywa chako, Baraza limekutia hatiani. Unaweza kwenda,” alisema Mhe. Teemba.
Baraza hili limefanyika chini ya Mwenyekiti wake Jaji (Mst.) Rose Teemba, akisaidiana na Wajumbe wa Baraza hilo Bw. Peter Ilomo na Bi. Suzan Mlawi.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Emma Gelani, Bw. Hassan Mayunga, Bw. Hillary Hassan, Lydia Mwakibete na Catherine Tibasana.
Kikao hicho cha Baraza kimeahirishwa hadi tarehe 28 Machi 2025 ambapo walalamikiwa wengine watatu akiwemo Mhe. Sakina Jumanne Mohamed, Mkuu wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita watafikishwa mbele ya Baraza.