VIONGOZI ONGEZENI UWAZI, UWAJIBIKAJI KWA WANANCHI KUCHOCHEA MAENDLEO.
Viongozi wa Umma nchini wametakiwa kuongeza kasi ya utendaji kazi, kuchochea maendeleo kwa wananchi na kuzingatia maadili, uwazi na uwajibikaji wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bi. Doris Ntuli Kalasa wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa Taasisi mbalimbali za mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA tarehe 17 Mei 2024.
Bi. Doris alisema kuwa maadili ndio kinga ya maozo yote katika jamii na ndio chimbuko la mafanikio katika maeneo mbalimbali kama vile elimu, maji, kijamii, kiutamaduni pamoja na kukuza utawala bora.
“Kiongozi wa umma anatakiwa kubadilika kimtazamo na kifikra na kuzingatia kwa vitendo swala la maadili kwa kuwa kiongozi wa umma ni kioo cha jamii popote pale anapokuwepo,” alisema, Bi. Doris Kalasa na kuongeza kuwa, “ndio maana kila wakati tunamsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akisisitiza Maadili kwa Viongozi wa Umma.”
Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, amewaagiza viongozi wa umma waliopata mafunzo kuandaa utaratibu wa kuyafikisha mafunzo kwa watumishi wote walio chini yao na maeneo wanayosimamia ili kulahisisha majukumu yao ya kila siku na kupunguza matukio ya uvunjifu wa maadili kwenye ofisi za umma.
“Naishukuru Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuandaa mafunzo ambayo yatawasaidia Viongozi wa Iringa kujijenga kimaadili na kuwakumbusha wakati wote misingi ya maadili wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao,” Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa alisema.
Kwa upande wake Bw. Salvatory Kilasara, Katibu Msaidizi, Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya maadili amewatoa hofu viongozi wa umma kuhusu ujazaji Tamko la Rasilimali na Madeni kuwa halina maana ya kuzuia kiongozi wa umma kumiliki mali.
Amesema, “kiongozi wa Umma haki ya kumiliki mali ila iwe ni mali halali.”
Bw. Kilasara amesema msingi wa mafanikio kwa kiongozi wa umma ni nidhamu na maadili ili kuondoa migongano na migogoro ya kazini na kuhakikisha kiongozi wa umma unaishi maisha yako na kurizika na unachopata na epuka kuishi Maisha ya watu wengine.