Viongozi na Watumishi watakiwa kuwajibika:

Viongozi na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze wametakiwa kufanya kazi kwa kuwajibika kwa pamoja na kujiepusha na mgongano wa Maslahi, katika utendaji wao wa kila siku.
Kauli hiyo, imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Archanus Kilaja alipokuwa akifungua mafunzo ya Maadili kwa viongozi na watumishi wa halmashauri hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo tarehe 23 Mei, 2023.
Aidha, Bwana Kilaja katika hotuba yake aliwaasa viongozi na watumishi hao, kuyaishi na kuyafanyia kazi yale yote waliojifunza katika kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
Bwana Kilaja ameiomba Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa mafunzo ya maadili kwa watumishi wengine wa Halmashauri hiyo ikiwemo idara ya Afya, Watendaji wa Kata na Vijiji na kwamba hao ndiyo wanaolalamikiwa zaidi na wananchi kukiuka maadili.
Naye Katibu Msaidizi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam Bi. Elizaberth Komba amewataka Viongozi na watumishi hao waliopata mafunzo kuwa mabalozi wazuri na kuwaeleza watumishi wenzao ambao hawakubahatika kupata mafunzo hayo kuyatekeleza yote waliojifunza ili kuleta ufanisi kazini.
Bi. Komba aliwataka viongozi hao kuyaishi yale yote waliofundishwa na kuyatekeleza katika maeneo yao ya kazi ili kuleta tija katika utendaji wao wa kazi za kila siku na kuongeza uwajibikaji, uwazi na uzalendo ambao utachangia katika kuboresha wao wa utendaji kazi.
Mafunzo hayo ya siku moja, yamewashirikisha Viongozi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze takribani 100.