Viongozi na Watumishi wa Misenyi wasisitizwa kufanya kazi kwa Ushirikiano

Viongozi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera wasisitizwa kufanya kazi kwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa nafasi mbalimbali za utumishi walizo nazo ili kuleta tija katika Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Mhe.Wilson Sakulo alipokua akifungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi na watumishi wa Umma waHalmashauri ya Wilaya ya Misenyi iliyopo Mkoani Kagera. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo tarehe 24 Oktoba,2023.
Katika hotuba yake Mhe. Wilson alisema kuwa uwajibikaji wa pamoja kwa Viongozi na watumishi wa Umma ni jambo muhimu sana kwani kutokuepo kwa ushirikiano na maelewano kwa Viongozi na watumishi wa Umma kunarudisha nyuma na kukwamisha shughuli za maendeleo ya Halmashauri, Wilaya, Taasisi na hata Serikali kwa ujumla.
“Mara nyingi tumeona kutokuepo kwa maelewano kati ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi ama Mkuu wa Idara na Mkurugenzi jambo ambalo ni utomvu wa maadili na halitakiwi kujitokeza katika Wilaya yetu ya Misenyi, tunatakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana kwani umoja ni nguvu bali utengano ni udhaifu, tusiposhikamana lazima kuna mahali tutakwama” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Wilson alieleza kuwa suala la mgongano wa maslahi limekua likiathiri ufanisikwenye utendaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali. “Kumekua na baadhi ya Viongozi na watendaji wasio waadilifu wamekuwa wakijiingiza kwenye mgongano wa maslahi kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi, familia zao, jamaa na marafiki zao, Jambo hili limekua likisababisha kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi pamoja na kuzorotesha utoaji wa huduma kwa jamii”alisema.
Aidha Mhe. Wilson alitoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kwamba elimu watakayoipata ikalete mabadiliko katika mienendo yao na kukuza nidhamu uadilifuna uwajibikaji ili kuweza kuleta ufanisi wa utolewaaji wa huduma katika maeneo yao ya kazi ili kutimiza lengo la Serikali la kuinua maisha ya wananchi kiuchumi.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Katibu Msaidizi Kanda ya Ziwa-Mwanza Bw, Godson Kweka alisema kuwa lengo la Sekretarieti ya Maadili kufanya mafunzo hayo katika Wilaya ya Misenyini kutokana na Halmashauri hiyo kukumbwa na changamoto nyingi zinazosababishwa na ukiukwaji wa Maadili.
Bw. Kweka aliendelea kusema kuwa Viongozi na Watumishi wa Ummakatika Halmashauri hiyo wameshindwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia rasilimali za Halmashauri hali inayopelekea ufinyu na upotevu wa mapato ya Halmashauri hiyo.
“Sote tunafahamu jinsi Halmashauri yenu inavyopoteza mapato mengi katika vyanzo vyake vingi hasa katika masoko na tumeona Viongozi wetu wa ngazi za juu wakizungumza kuhusu suala hilo hivyo sisi kama Taasisi inayosimamia maadili tumekuja kuwakumbusha kuwawote mnaosimamia vyanzo hivyo ni Viongozi na watumishi wa Umma mnaoongozwa na Sheria na kanuni mbalimbali za nchi hivyo mnapaswa kuwa waadilifu kwa kuzingatia na kuviishi viapo vyenu ”alisema
Aidha Bw, Kweka aliwasisitiza Viongozi na watumishi hao kuhakikisha kuwa wanalindana kujenga utamaduni wa kuzingatiamaadilikatika maeneo yao ya kazi hali itakayojenga Imani ya wananchi kwa watumishi hao na serikali kwa ujumla
“Tunahitaji Viongozi na watumishi waadilifu katika Halmashauri ya Misenyi watakaoweza kusimamia rasilimali za Halmashauri kwa manufaa ya wananchi na Serikali kwa ujumla na sio kwa manufaa yao binafsi” alisema.
Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewa kwa Madiwani, Wakuu wa Divisheni na Vitengo, Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali, Watendaji wa Kata pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi
Aidha mada tatu ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, mada kuhusu uwajibikaji wa pamoja na mada iliyohusu Mgongano wa maslahi