JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

PO-ETHICS SECRETARIAT Logo
VIONGOZI KANDA YA MAGHARIBI WAPIGWA MSASA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
12 Feb, 2026
VIONGOZI KANDA YA MAGHARIBI WAPIGWA MSASA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Viongozi mbalimbali wa Umma ambao ni Wakuu wa Idara/Kitengo cha TEHAMA kutoka Halmashauri za Wilaya, Manispaa na miji katika Kanda ya Magharibi wapatiwa mafunzo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Grand Penta Hotel mkoani Tabora tarehe 12 Februari, 2026. Akifungua mafunzo hayo Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi-Tabora Bi. Anna Mbasha alisema kuwa lengo la kuratibu mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi juu ya uzingatiaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya mwaka 1996 katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Viongozi wenzangu tumekuja hapa kukumbushana juu ya Sheria ya Maadili itusaidie katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku kama Viongozi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu pamoja na kuzingatia misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma” alisema.

Aidha Bi. Mbasha alieleza kuwa suala la kuzingatia maadili kwa Viongozi wa Umma ni muhimu kwa sababu maadili ndio msingi wa uongozi bora na unao aminika kwa wananchi kwani sheria inawataka viongozi kufanya kazi kwa maslahi ya umma badala ya maslahi yao binafsi.

“Wananchi wanamategemeo makubwa sana kwa Serikali yao na nyinyi kama viongozi wa Halmashauri ndio watekelezaji  wa mikakati yote ya Serikali msipozingatia sheria kwa kufanya maamuzi ya haki na yenye kuzingatia maslahi ya wananchi lazima mtakwaruzana na wananchi watakosa Imani na Serikali yao” alisema.

Katika hatua nyingine Bi. Mbasha alieleza kuwa katika mafunzo hayo pia Viongozi watapatiwa elimu ya namna ya utumiaji wa mfumo wa ujazaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya mtandao (ODS) “Kama tunavyojua sasa hivi Viongozi wote wanajaza Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya mtandao hivyo tumeona kuwa upo umuhimu wa kuwaelekeza namna ya matumizi sahihi ya mfumo huu ilikufanya zoezi hili kuwa rahisi na rafiki kwetu sote” alisema.

Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Maadili Afisa Maadili Bw. Patrick Shayo alieleza juu ya misingi ya maadili ya Viongozi wa Umma ambayo ni pamoja na ­Kujiepusha na mgongano wa maslahi, kufanya maamuzi kwa kuzingatia misingi ya sheria, kanuni na taratibu, kujiepusha na kupokea zawadi, kutoa Tamko la Rasilimali maslahi na madeni, kutenda haki, kutumia taarifa za ofisi kwa manufaa binafsi, kutoa taarifa za kiofisi kwa watu wasiohusika.

“Ni kosa la kisheria kiongozi akishindwa kuzingatia misingi ya Maadili na adhabu yake ni kwa mujibu wakifungu cha 8 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambazo ni pamoja na kushushwa cheo, kusimamishwa, ama kufukuzwa kazi, kushauriwa kujiuuzulu pamoja na adhabu nyingine mbalimbali” alisema.

Viongozi walioshiriki mafunzo hayo yaliyokua na lengo la kuwakumbusha masuala mazima ya uadilifu kwa Viongozi wa Umma ni Wakuu wa Idara na Kitengo cha TEHAMA kutoka Kanda ya Magharibi.

 

 

 

 

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >