Viongozi Geita wasisitizwa matumizi ya ODS katika kujaza Tamko la Rasilimali na Madeni
Viongozi mkoani Geita wametakiwa kutohofia matumizi ya mfumo wa ujazaji wa Tamko la Rasimali na Madeni kwa njia ya mtandao (Online Declaration System-ODS) kwani mfumo huo ni rafiki katika kutunza taarifa za mtumiaji.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa Viongozi wa Mkoa huo yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa na kufanyika katika ukumbi wa mikuatno wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 20 Februari, 2026.
“Utaratibu wa kujaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kiongozi wa Umma umewekwa kwa mujibu wa Sheria kwa Kiongozi wa Umma kujaza mali zake, na sio vinginevyo, hivyo tusiwe na hofu katika kuutumia, kwani ni mfumo mzuri hasa katika kutunza taarifa za mtumiaji,” alisema Mhe. Shigela.
Aidha Mhe. Shigela ametumia nafasi hiyo kuishukuru Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kuendelea kuwa nao bega kwa bega kwa kuandaa semina za mara kwa mara za maadili na amewasisitiza Viongozi wa Mkoa huo kutumia semina hizo kurekebisha sehemu zenye mapungufu kwa lengo la kuimarisha ustawi wa Mkoa huo na wananchi wake.
“Tumekua tukipatiwa semina hizi kwa nyakati tofauti na mara nyingi wanakutumbusha kuwajibika kwa kufuata Sheria na kanuni zilizopo katika utumishi wa umma, hivyo ni wakati sahihi sasa kutumia semina hizi katika kuboresha sehemu zenye mapungufu kwa kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu,” aliongeza.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa Bw. Godson Kweka amewataka Viongozi wa Mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, kuepuka mgongano wa maslahi na kufanya kazi bila upendeleo.
“Tusifanye kazi kwa upendeleo, ubinafsi na pia tujitaidi katika kutunza taarifa za ofisi na kuepuka vitendo vya rushwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi,” aliongeza Bw. Kweka.
Viongozi walioshiriki mafunzo hayo ni pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Wilaya, Madiwani na Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita.
