Uongozi wenye Maadili huimarisha Imani ya wananchi kwa serikali.
Uongozi wenye Maadili huimarisha Imani ya wananchi kwa Taasisi za Umma na serikali kwa ujumla. Wananchi wanapowaona Viongozi wao wakitenda kwa haki, uwazi na uadilifu huongeza ushirikiano, utii wa sheria na mshikamano katika jamii inayowazunguka.
Hayo yalisemwa na Mhe. Mathew Kirama Katibu na Mtendaji Mstaafu, Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma akimuwakilisha Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi , Kamishna wa Maadili alipokua akifungua mafunzo ya maadili kwa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Makatibu Tawala wasaidizi wa mikoa na Makatibu Tawala wa wilaya . Mfunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa hoteli ya Morena-Morogoro tarehe 15 Aprili,2026.
Katika hotuba yake Mhe. Kirama alisema kuwa katika mazingira ya sasa ya Utumishi wa umma maadili kwa Viongozi ni suala muhimu sana kwani kuna mtanziko mkubwa wa changamoto za kimaadili kuanzia ngazi ya familia, taasisi za umma na jamii kwa ujumla. Hivyo Viongozi wanapaswa kuwa mfano mzuri wa uzingatiaji wa maadili ili kuimarisha utawala bora na kuwa chachu ya maendeleo kwa serikali.
“Viongozi wa Umma mnatarajiwa kuwa kielelezo kizuri cha uaminifu, uwazi, usawa na uzingatiaji wa sheria katika maamuzi yenu ya kila siku ili kujenga Imani ya wananchi kwenu na serikali yao kwa ujumla” alisema.
Mhe. Kirama aliendelea kusema kuwa maadili si suala la hiari bali ni suala la lazima na msingi wa uongozi bora na utendaji wenye tija kwa watumishi na Viongozi wa umma. Maadili husaidia kuzuia migongano ya maslahi, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na upendeleo na mambo mengine kama hayo.
“Maadili hujenga utamaduni wa kuwajibika, huimarisha nidhamu ya kiutumishi na huogeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya viongozi kwa umma “ alisema.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo Mhe. Glory Absalum, Katibu Tawala –Kahama alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa viongozi hao kwani wao kama wasimamizi wa rasilimali za nchi wanatakiwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora kutoka kwa serikali yao.
“Niwasihi Viongozi na watumishi wenzangu kuhudhuria mafunzo haya ambayo tumeambiwa yana muendelezo kwa mujibu wa ratiba yao kwani mafunzo haya yanatukumbusha majukumu yetu mbalimbali ambayo sisi kama viongozi tunapaswa tukayasimamie na yatatupa nyenzo muhimu katika utendaji kazi wetu” alisema.
Mafunzo hayo ya siku tatu ni matokeo ya ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha ambapo moja ya lengo la ushirikiano huo ni kutoa mafunzo ya maadili na utawala bora kwa Viongozi wa Umma.
Mafunzo hayo ya maadili yataendelea kufanyika kwa mwezi Aprili – Juni, 2026 ambapo kutakua na mafunzo ya Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Taasisi za Umma na Wakurugenzi wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma tarehe 22-24 Aprili,2026 Jijini Arusha, Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma tarehe 03 -05 Mei,2026 Jijini Mwanza, Wakuu wa Idara na Vitengo katika Wizara, Idara za Serikali Taasisi za Umma, Mamlaka za Serikali na Mashirika ya Umma tarehe 10-12 Juni,2026 Jijini Arusha na 24-26 Juni,2026 Jijini Mwanza.
