Ujumbe kutoka Tume ya Maadili Zanzibar
Ujumbe kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar wafanya ziara Sekretarieti ya Maadili
Ujumbe kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar ukiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Balozi Dkt. Mahadh Juma Maalim wafanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma makao makuu Dodoma tarehe 07 Oktoba,2026..
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Tume hiyo alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kubadilishana uzoefu wa namna ya utendaji kazi kwa Taasisi hizo mbili kwani zinatekeleza majukumu sawa na yanayofanana.
“Tumekuja kujitambulisha kwenu , kujifunza na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wetu kwani sote tunatekeleza majukumu mamoja na lengo kuu has ani kuendelea kukuza ushirikiano wetu ambao umekuwepo kwa muda mrefu” alisema.
Aidha, Balozi katika hotuba yake alifafanua kuwa kumekuwepo na makubaliano ya ushirikiano wa pamoja katika Nyanja mbalimbali kati ya Taasisi hizo mbili lakini makubaliano mengi hayajatekelezwa hivyo ni wakati muafaka wa kuyatekeleza ili kuleta tija kwa serikali na kwa wananchi kwa ujumla.
“Niwaahidi kushirikiana nanyi kwa karibuna tusiridhike na makubaliano tuliyoyaandika tuu bali sisi kama viongozi tuwe na utashi na utayari wa kuyatekeleza kwa vitendo ili kuiimarisha ushirikiano huu” alisema.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Tume hiyo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi aliwashukuru wajumbe hao kwa ziara hiyo ambapo pia aliyataja baadhi ya Majukumu yanayotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo ni pamoja na kupokea matamko ya rasilimali na madeni yanayotakiwa kutolewa na Viongozi wa Umma , kupokea taarifa na tuhuma za ukiukwaji wa Sheria, kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa Sheria, kufanya uhakiki wa matamko yaliyotolewa kwa mujibu wa Sheria, kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote wa tuhuma za ukiukwaji wa maadili yaliyobainishwa na Sheria,kutoa elimu ya maadili kwa Viongozi wa Umma, nakadhalika.
Ziara hiyo iliwakutanisha wajumbe wa Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao pia ni wakuu wa idara na vitengo ambao walipata fursa ya kuchangia masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano huo wa Taasisi hizo mbili katika utekelezaji wa makukumu yao.
