Simbachawene: Tujikite katika kuzuia rushwa badala ya kupambana madhara yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amezitaka taasisi zinazohusika na kusimamia utawala bora nchini, kujikita Zaidi katika kuzuia vitendo vya rushwa hususani kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo badala ya kusubiria mpaka rushwa itokee ndipo wanaanza kupambana nayo.
“Wakati mwingine tunaweka nguvu kubwa na rasilimali nyingi katika kupambana na rushwa wakati ambapo matokeo ya rushwa yanakua tayari yameshatokea na kuleta madhara kwa serikali badala yake tulipaswa kutumia nguvu hiyo hiyo katika kuzuia rushwa isiweze kutokea” alisema.
Mhe. Simbachawene alisema hayo kwenye kongamano la jukwaa la kitaifa la wadau wa juhudi dhidi ya rushwa lililofanyika tarehe 04 Desemba , 2023 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maadili na haki za binadamu nchini ambapo kilele chake ni tarehe 10 Desemba,2023. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Zingatia Maadili, Utu, Uhuru, na Haki kwa watu wote kwa maendeleo endelevu”
Katika hotuba yake Mhe. Simbachawene alibainisha kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini ikiwemo tafiti kuhusu hali ya ya Utawala Bora nchini zimebaini kuwa rushwa ni mojawapo ya changamoto katika ufikiwaji wa lengo la serikali la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu, maji na nk.
“Niwahakikishieni Serikali yetu haitaacha kukabiliana na vitendo vya rushwa na kupambana inapobidi kwa kuwa zipo njia mbalimbali za kuzuia rushwa isiweze kutokea mojawapo ni hii ya kujadili pamoja mbinu za kuboresha zaidi usimamizi wa miradi ya maendeleo” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene alieleza kuwa matarajio ya Serikali kupitia mdahalo huo ni kupata mbinu mpya na mawazo mapya ya namna ya kuweza kupambana na rushwa ili kuweza kukuza Maadili nchini .
“Ni Imani yangu kuwa wadau wa sekta zote kwa umoja wetu tutatenda haki kwa mada zitakazowasilisha kwenye jukwaa ili kuweza kutoka na maazimio yatakayosaidia juhudi za kuzuia Rushwa badala ya kusubiri na kupambana wakati tumeshapoteza rasilimali nyingi” alisema.
Awali akitoa neno la utangulizi Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ambaepia ni mwenyekiti wa maadhimisho hayo Mhe. Jaji (Mst) Sivangilwa Mwagesi alisema kuwa
moja kati ya shughuli zilizopanga kutekelezwa katika maadhimisho ya mwaka huu ni Jukwaa la kitaifa la Wadau wa Juhudi ya Rushwa ambalo linakutanisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Umma watakao jadili kwa kina kuhusu uadilifu wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Jaji (Mst) Sivangilwa Mwagesi alieleza kuwa kila tarehe 10 desemba, Tanzania huungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha siku ya Haki za Binadamu Kimataifa ambalo chimbuko lake ni tamko la Haki za Binadamu liililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tarehe 10 Desemba, 1948 (Universal Declaration of Human Rights - UDHR).
Siku ya Maadili na Haki za Binadamu hapa nchini ilianza kuadhimishwa kwa pamoja mwaka 2016 ikiwa ni muunganiko wa siku mbili yaani siku ya Maadili na Haki za Binadamu.
Maadhimisho hayo huratibiwa na taasisi zinazosimamia utawala bora ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.