Simbachawene azindua wiki ya maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachewe (Mb) amezindua wiki ya maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa kwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini. Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 05 Disemba,2024 katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Jijini Dodoma.
Mhe. Simbachawene katika hotuba yake alifafanua kuwa maadhimisho hayo ni utekelezaji wa muunganiko wa siku mbili kitaifa ambazo ni siku ya Maadili na Haki za Biinadamu inayoadhimishwa Disemba 10 ya kila mwaka pamoja na siku ya mapambano dhidi ya rushwa ambayo huadhimishwa kila tarehe 9 Disemba ya kila mwaka,
Serikali ya Tanzania iliamua kuunganisha utaratibu wa Maadhimisho ya siku hizo mbili na hivyo kuifanya tarehe 10 Desemba kila mwaka kuwa siku ya Maadili na Haki za Binadamu.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo siku ha maadili na haki za binadamu kwa mwaka 2024 ni Tumia haki yako ya kidemokrasia chagua Viongozi waadilifu na wanaozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa maendeleo ya Taifa.
Mhe. Simbachawene alifafanua kuwa katika kilele cha Maadhimisho ya Siku hiyo kwa mwaka 2024 kutakuwa na kongamano la watoa huduma ambao ni watumishi wa umma litakalofanyika katika ukumbi wa PSSF Makole tarehe 10 Disemba,2024
“Lengo la kufanya kongamano hilo kwa watumishi wa umma ni kutoa fursa kwa watumishi wa umma kujitathmini namna wanavyotoa huduma kwa kuzingatiia Maadili na Haki za Binadamu na jinsi wanavyoweza kuepuka vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi” alisema.
Katika kongamano hilo mada mbili zitawasilishwa na kujadiliwa ambazo ni Haki za binadamu katika mapambano dhidi ya rushwa na mada ya pili ni Maadili haki na wajibu wa watumishi wa Umma.
Maadhimisho hayo yanaratibiwa na Taasisi zinazosimamia Utawala Bora nchini ambazo ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.