Sekretarieti ya Maadili yafungua Klabu za Maadili wilayani Manyoni

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia Kanda ya Kati, Dodoma, imefungua Klabu mpya 10 pamoja na kuhuisha klabu 06 za Maadili katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida ili kuwaandaa na kuwajengea wanafunzi uzalendo na uadilifu kwa Taifa letu.
Zoezi la uanzishaji wa klabu za Maadili lilifanyika kati ya tarehe 22 hadi 25 Aprili, 2025 katika shule za msingi za msingi na sekondari.
Shule za msingi zilizoanzisha klabu mpya za maadili ni Mbwasa, Sukamajela, Sayuni, Solya, Muhalala , Umoja, National, na sekondari ni Solya, Mtori na Mwanzi. Aidha klabu zilizohuishwa ni pamoja na klabu ya shule ya msingi Bomani, Manyoni, Mwembeni, Majengo,Tambukareli na kwa upande wa sekondari ilihuishwa klabu ya shule ya Manyoni.
Akizungumza wakati wa uanzishwaji na uhuishwaji wa klabu hizo Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili Bw. Christian Kapere alisema kuwa Taasisi imeona ni vyema kuanzisha klabu za maadili katika taasisi za elimu na kuhuisha klabu ambazo zilikua hazifanyi vizuri ili kukuza kizazi na jamii adilifu.
“Tumekuja kuanzisha klabu za Maadili katika shule hizi tukiamini kwamba Viongozi watakaoongoza Taifa hili hapo baadaye wapo miongozi mwenu. Hivyo, ni dhahiri kuwa mnapaswa kupewa elimu ya maadili ili kuwandaa kuwa viongozi waadilifu na wazalendo mtakaofanya maamuzi kwa manufaa ya jamii nzima,” alisema.
Bw, Kapere alieleza kuwa klabu za Maadili katika ngazi za shule za msingi, sekondari na vyuo zina umuhimu mkubwa kwani elimu inayotolewa, itasaidia kuwajengea wanafunzi misingi bora ya maadili mapema na kuzuia vitendo vya mmomonyoko wa maadili
Miongoni mwa mambo muhimu yanayofundishwa katika klabu za Maadili ni uwajibikaji, uzalendo, heshima, kujali watu wengine, kusema ukweli na kuwa mzalendo kwa nchi yako.
“Sote tunafahamu kuwa malezi yanachangia kwa asilimia kubwa kuamua hatma ya watoto wetu hapo baadae, ndio maana waswahili wanasema, samaki mkunje angali mbichi, basi nasi tumekuja kuanzisha klabu hizi ili tuweze kutoa elimu hii ya maadili tukiamini kuwa watoto hawa watakua na kuishi nayo mpaka watakapokua wakubwa,” alisema.
Katika hatua nyingine Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Mbwasi wilayani Manyoni ambae pia ni mlezi wa klabu ya Maadili shuleni hapo Mwl. Anna Minja alisema kuwa klabu hizo zitakua na manufaa makubwa shuleni hapo kwani zitasaidia wanafunzi kuishi kwa kuzingaia misingi bora ya uadilifu na kuongeza ufaulu katika masomo yao.
“Kwa upande wetu, tumefarijika sana na uanzishwaji wa klabu za Maadili kwani zitatusaidia kujengea wanafunzi wetu misingi bora itakayosaidia kuongeza uadilifu na kukuza ufaulu kwa wanafunzi wetu.”
“Sisi tutajitahidi kutoa elimu ili kuhakikisha klabu hizi zinafanikiwa na kuleta mabadiliko katika jamii yetu,” alisema.