Sekretarieti ya Maadili yafanya Mdahalo kuhusu masuala ya Maadili kwa wanafunzi

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imefanya Mdahalo na wadau mbalimbali wa masuala ya maadili kuhusu changamoto za kimaadili kwa wanafunzi katika shule za msingi, sekondari na vyuo.
Mdahalo huo uliofanyika tarehe 26 Agosti, 2025 katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha ulihusisha wadau mbalimbali wa maadili wilayani humo.
Wadau walioshiriki katika mdahalo huo ni jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Wakuu wa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Halmashauri, Waalimu Wakuu na Walezi kutoka shule za Msingi na Sekondari, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vitongoji pamoja na wadau wengine.
Katika Mdahalo huo baadhi ya wadau walipata fursa ya kuchangia namna ya kukuza uadilifu miongoni mwa wanafunzi katika halmashauri ya wilaya ya Meru ambapo Mwalimu Mkuu Shule ya msingi Elerai Bi. Julieth Malisa wakati akichangia mada alisema kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili ni mazingira anapoishi mtoto kuwa baadhi ya mazingira sio rafiki kwa watoto na watoto wana tabia ya kuiga wanavyoviona.
“Utakuta mzazi ni mlevi akirudi nyumbani anawatukana watoto na tabia nyingine mbaya mtoto anapoona anajua haya ndio maisha na yeye anakuwa hivyo hivyo,” alisema.
Mwl. Julieth alitoa rai kwa waalimu na kuwataka kuwa karibu na wanafunzi ili waweze kusema changamoto wanazokutana nazo nyumbani na mtaani.
Bw. Selemali Alba, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Sakila alieleza kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili ni kupoteza hofu ya Mungu.
“Kwa sasa jamii haina hofu ya Mungu ndio maana unakuta binadamu anafanya kitu ambacho kila mtu anashangaa hatuogopi tena, tumrudie Mungu ili tuishi katika maadili mema,” alisema.
Katika hatua nyingine Terewaeli Kaaya, Mwalimu mlezi Shule ya Msingi Patandi alisema kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili ni baadhi ya jamii kumaliza mambo nyumbani.
“Sisi kama waalimu tunakutana na changamoto za watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili, tunashirikiana na mtoto kuripoti katika vyombo husika baada ya muda familia inaamua kukutana na watuhumiwa wanawapa hela kidogo wanayamaliza. Kwa namna hii haya hawezi kuisha ni lazima tuwafundishe wazazi kuacha sheria husika ichukue mkondo wake, “ alisema.
Naye mkuu wa dawati la Jinsia Wilayani Arumeru Insp. Salama Ally alisisitiza walimu wa malezi kutafuta taarifa zinazohusiana na utovu wa maadili shuleni badala ya kusubiri kuletewa na wafuatilie mienendo ya kesi badala ya kukaa kulaumu jeshi la polisi.
Akifungua mdahalo huo Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini Bw, Gerald Mwaitebele alisema kuwa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeamua kufanya mdahalo huo baada ya kuibuka kwa changamoto za kimaadili wakati Ofisi hiyo ikifungua klabu za maadili shuleni.
“Tulikuwa na zoezi la kufungua klabu za maadili shuleni, huko tulikutana na changamoto nyingi wanazokumbana nazo watoto wetu kama vile kukosa uadilifu, matumizi ya dawa za kulevya, utoro na nyingine nyingi, ndio maana tukaona tukae meza moja na nyinyi tujadili kwa pamoja ili tutoke na maazimio ambayo lazima tukayatekeleze kwa manufaa ya watoto wetu.”
Aidha Bw, Mwaitebele alisisitiza kuwa jukumu la kulea watoto sio la walimu peke yao bali la jamii nzima inayotuzunguka
“Ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kulea na kuhakikisha watoto wako salama na kuwapatia mahitaji yao muhimu,“ alisema.
Katika mdahalo huo wadau waliazimia yafuatayo: kutoa elimu kwa wazazi na walezi, uwepo wa vikao vya mara kwa mara katika ngazi za chini za uongozi na kuweka sheria kali dhidi ya wanaokiuka maadili, ushirikishwaji wa viongozi wa dini na viongozi wa mila katika kukuza maadili pamoja na kuitisha vikao vya wazazi shuleni na kuwaalika wadau mbalimbali wa masuala ya elimu na maadili ili kushirikiana kutoa elimu kwa pamoja.