Sekretarieti ya Maadili yaanza kazi ya marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,1995

Sekretarieti ya Maadili yaanza kazi ya marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,1995
Sekretarieti ya Maadili imeanza kazi ya kufanya marekebisho ya Kanuni za sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995, Katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Edema mkoani Morogoro kuanzia tarehe 06 Juni 2022 hadi tarehe10 Juni 2022.
Akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi ,Katibu Idara ya Ukuzaji Maadili Sekretarieti ya Maadili Bw. Waziri Kipacha alisema kuwa kazi hii ya urekebu wa kanuni za Maadili inafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Bw. Kipacha alieleza kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma tokea kutungwa kwake mwaka 1995 imetungiwa kanuni zipatazo nne pamoja na kutolewa matangazo ya Serikali mawili kwa lengo la kuongeza ufanisi na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti ya Maadili.
Aidha Bw. Kipacha aliongeza kuwa Kanuni hizo ni Pamoja na Kanuni za Tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni za mwaka 1996,Kanuni za Mwenendo wa Uchunguzi katika Baraza la Maadili za mwaka 2017, Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi za mwaka 2020 na Kanuni za Ahadi ya Uadilifu za mwaka 2020.
“ Kwa kuwa yemekwisha fanyika marekebisho ya Sheria mwaka 2001 na mwaka 2016 na pia kufanyika kwa marejeo hadi mwaka 2020 na kuibuka kwa mahitaji mapya ya Taasisi , Sekretarieti inalazimika kufanya marekebisho katika kanuni zate tajwa ili kuendana na mahitaji ya Taasisi kwa wakati ulipo” alisema Bw. Kipacha
Bw, Kipacha alitoa wito kwa washiriki wa kikao kazi hicho kushiriki kikamilifu na kutoa michango muhimu katika kazi hiyo kwani washiriki hao ni wazoefu na wabobevu wa fani ya sheria na ni sehemu ya watekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kanuni zake zote.
“Nawakumbusha kuwa kazi hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Mapambano dhidi ya Rushwa, awamu ya 111( NASCSAP-111), na hivyo ni sehemu ya kipimo kwa Taasisi yetu katikautekelezaji wa mpango huo na baadae tutatolea taarifa ya utekelezaji kwenye mamlaka husika” alifafanua Bw. Kipacha.
Kazi hii yamarekebisho ya Kanuni za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995 itakua na faida kubwa kwa Taasisi kwani kinachofanyika kinaenda kurahisisha na kuimarisha utendaji kazi wa Taasisi na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.