JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA YATAKIWA KUTUMIA MBINU ZA KISASA ZA UCHUNGUZI WA MALALAMIKO DHIDI YA VIONGOZI.
26 Nov, 2025
SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA YATAKIWA KUTUMIA MBINU ZA KISASA ZA UCHUNGUZI WA MALALAMIKO DHIDI YA VIONGOZI.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetakiwa kutumia mbinu za kisasa za uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu za utafiti, kuchunguza na kutoa elimu ya uadilifu kwa umma ili kupunguza mmomonyoko wa maadili nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi  katika ofisi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu jijini Dodoma tarehe 26 Novemba, 2025 ikiwa ni  mara yake ya kwanza kutembelea Taasisi hiyo tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo. Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri aliambatana na Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray (Mb).

“Shirikianeni na Taasisi nyingine za Utawala Bora nchini kufanya utafiti wa hali ya maadili nchini na kutoa elimu ya uzalendo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kupunguza mmomonyoko wa maadili, “ amesema.

Aidha Mhe. Kikwete ameiagiza Sekretarieti ya Maadili  kutowaonea  aibu Viongozi wa Umma wanaolalamikiwa kukiuka maadili kwa sababu ni jukumu lake kufuatilia tabia na mienendo ya Viongozi nchini.

“Sekretarieti ya Maadili ni msumeno wenye ncha kali, utumieni kuongeza uadilifu nchini kwa kutafuta ushahidi wa ukiukaji wa maadili miongoni mwa Viongozi wa Umma, waiteni  wanaokiuka maadili na wakemeeni wanaobainika kukiuka misingi ya maadili kwasababu hili liko katika mamlaka yenu,” amesema Mhe. Kikwete.

“Mmesema hapa kuwa kuna baadhi ya viongozi wana hofu ya kujaza Tamko kwa njia ya Mtandao, hili sio tatizo la Serikali, mmesha weka mifumo ya kupokea Tamko la Rasilimali na Madeni hakikisheni Viongozi wote wanajaza ifikapo tarehe 31 Desemba kwa mujibu wa sheria,”  amesisitiza.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma ni chombo  imara na kinaaminika hivyo kinatakiwa  kufanya kazi kwa kutenda haki kinapotekeleza majukumu yake ya kimsingi katika kusimamia na kukuza maadili kwa Viongozi wa Umma nchini.

Awali akimkaribisha Waziri, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi ameeleza kuwa Sekretarieti ya Maadili katika kutekeleza majukumu yake, inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kukosekana kwa ushahidi wa baadhi ya malalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya Viongozi kutokana na baadhi ya mashahidi kutotaka kutoa ushahidi mbele ya Baraza la Maadili.

Katika hatua nyingine, Mhe Mwangesi ameeleza kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuanzisha ofisi za  Mikoa ili kusogeza huduma kwa Viongozi wa Umma na wananchi hasa utoaji wa elimu ya Mgongano wa Maslahi.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >