Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yahitimisha wiki ya Utumishi wa Umma.

Katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili imefanya ziaraya kutembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Kijiji cha Matumaini pamoja na kufanya usafi katika Soko Kuu la Majengo lililopo jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wamekabidhi mahitaji mbalimbali katika Kituo cha watoto yatima zikiwemo sabuni na ‘pampers’ kwa watoto hao pamoja na vifaa vya kufanyia usafi kwa Soko Kuu la Majengo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Maadili wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Bw. John Kaole alisema, “Tumekuja kushirikiana na nyie kukuza Maadili ya jamii kwasababu maadili yanaanzia katika ngazi ya chini.”
Bw. Kaole aliongeza kuwa kituo hicho kinafanya kazi nzuri ya kuisaidia Sekretarieti ya Maadili kupata viongozi bora waliolelewa kwa kuzingatiamaadili.
Aidha Katibu huyo alifafanua kuwa watumishi wameguswa sana na kazi kubwa inayofanya na masista wa Shirika la ASC wanaotunza watoto hao yatima ndio maana wamekuja kuwapa faraja.
“Tunawapongeza sana Watawa mnaosimamia kituo hiki cha kijiji cha matumaini, mnalea watoto hawa kwa upendo, lakini zaidi ya yote mnawasaidia na kuwalea kwa upendo mkubwa na kuhakikisha wanapata mahitaji yote ya kijamii ikiwemo elimu,” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mkurugenzi wa kituo hicho Sr. Suzana Maingu alitoa shukrani kwa Sekretarieti ya Maadili kwa upendo mkubwa wa kuwatembelea na kujitoa kwa ajili ya watoto hao.
“Napenda kuishukuru Sekretarieti ya Maadili na nyote mliofika hapa kutoa msaada kila mmoja kwa nafsi yake kwa majitoleo yenu nakutambua uwepo wetu Mungu awabariki sana,” alisema.
Matembezi hayo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ambayo ilianza kuanzia tarehe 16 june ambapo kilele chake ni tarehe 23 Juni 2021 .