Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaanza kuitafsiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza kutekeleza kwa vitendo takwa la kisheria la kuitafsiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma linalotokana na marekebisho kwenye kifungu cha 84(1) na (2) cha Sheria ya Tafsiri za Sheria (Interpretation of Laws Act).
Kazi hiyo inayofanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Edema, mjini Morogoro kuanzia tarehe 27 – 31 Desemba, 2021.
Akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi, Katibu – Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya Maadili Bw. Waziri Kipacha alisema kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura ya 398 ilitungwa kwa lugha ya kingereza na hapakuwa na nakala rasmi iliyo kwenye lugha ya Kiswahili na hata iliyopo haikupitia utaratibu rasmi unaotamabulika.
Kwa mujibu wa Bw. Kipacha, mwaka huu yamefanyika marekebisho kwenye kifungu cha 84(1) na (2) cha Sheria ya Tafsiri za Sheria (Interpretation of Laws Act), Sura ya 1, kupitia kifungu cha 4 cha the Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, Na. 1 ya 2021 na kuagiza kuwa lugha ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitakuwa ni Kiswahili pamoja na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo kwa sasa zipo kwa lugha ya Kingereza zitatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
Bw. Kipacha aliendelea kubainisha kuwa kutokana na marekebisho hayo kuweka takwa la kufasiri Sheria zote kwenye lugha ya Kiswahili ikaonekana ni vema kufanya sasa kazi hii ya kutafsiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma sasa kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia Mradi wa kuzijengea uwezo Taasisi katika kupambana na rushwa nchini Tanzania.
Bw. Kipacha alitumia fursa hiyo kuwataka washiriki wa kazi hiyo ambao wengi wao niwanataaluma ya sheria kwa ngazi ya shahada na kuendelea, kutumia taaluma zao za sheria na kuwatumia vizuri Maafisa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kurugenzi ya Uandishi wa Sheria ili waweze kupata kitu kizuri.
“Nawakumbusha kuwa kazi hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Mapambano dhidi ya Rushwa, awamu ya III (NACSAP-III) hivyo ni sehemu ya kipimo kwa Taasisi yetu katika utekelezaji wa mapango huo na baadae tutatolea taarifa ya utekelezaji kwenye mamlaka husika” alifafanua Bw. Kipacha.
Uwepo wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lugha ya Kiswahili utawasaidia wadau wake hususani wananchi wa kawaida kuifahamu Sheria hii kwa lugha wanayoifahamu hivyo kuisaidia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kusimamia utekelezwaji wake.