Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kushirikiana na vyombo vya habari katika kukuza maadili
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imekutana na kufanya kikao kazi na wadau wa habari wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na waandishi wa habari wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa lengo la kuimarisha uhusiano katika kukuza maadili nchini.
Kikao kazi hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Midland iliyopo Makambako mkoani Njombe tarehe 30 Machi, 2026.
Akifungua hicho Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bw. Pauline Kanoni amesema lengo la kikao hicho ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuchakata na kuripoti habari zenye viashiria vya ukiukwaji wa maadili hasa kwa Viongozi wa Umma na pia kuimarisha uhusiano kati ya ofisi hiyo na vyombo vya habari vya mikoa hiyo.
“Tumewaita hapa kwa lengo la kujadiliana namna ya kuripoti habari kuhusu Viongozi wa Umma hasa wanapokiuka maadili katika uwajibikaji wao, maana vyombo vya habari ni nyenzo muhimu katika kutoa taarifa zenye viashiria vya ukiukwaji wa maadili, na pia ni mhimili katika kukuza uhusiano kati ya Serikali na wananchi,” alisema Bw. Kanoni.
Aidha Bw. Kanoni ameongeza kuwa katika ushirikiano huo vyombo vya habari vitanufaika katika kupata elimu ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia semina mbalimbali kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na wao vyombo vya habari watakua na jukumu la kuandaa na kutoa muda kwa ajili ya taarifa mbali mbali kuhusu uadilifu kwa Viongozi wa Umma na jamii kwa ujumla.
“Kama tunavyojua Serikali ina vyombo vyake vya habari, lakini tukitegemea vyombo hivyo pekee hatuwezi kufikia lengo la kuwajulisha wananchi kazi za Serikali yao kwa upana na kwa wakati ,hivyo kupitia ushirikiano huu tutawafikia wananchi wengi na wao kupata kujua yanayofanywa na Serikali yao,’’ aliongeza.
Akitoa neno la shukrani, mmiliki wa kituo cha redio ya Ice Fm iliyopo Makambako mkoani Njombe Dkt. Yono Kevela amesema kuwa wao kama wadau wa habari wamepokea vizuri ushirikiano huo na kuaidi kufanyia kazi yote waliokubaliana na kuomba vikao hivyo viwe endelevu.
“Tumefarijika kwa ujio wenu na tunashukuru kwa semina hii na tutafanya kazi kwa pamoja kwa ustawi mpana wa Taifa na sisi kama vyombo vya habari tutajaribu kufichua na kutoa habari za Viongozi wasiotenda haki kwa wananchi,” alisema Dkt. Kevela.
