Sekretarieti ya Maadili kushirikiana na Vyombo vya habari kukuza Maadili Nchini
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati - Dodoma imekutana na kufanya kikao kazi na wadau wa habari wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Sekretarieti na vyombo vya habari katika kukuza na kuimarisha maadili nchini.
Kikao kazi hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Zabibu Hotel iliyopo Mkoani Dodoma tarehe 01 Aprili, 2026.
Akifungua kikao kazi hicho Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kati Bi. Jasmin Awadh alieleza kuwa vyombo vya habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi na pia vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha maadili nchini kupitia redio, luninga, magazeti pamoja mitandao ya kijamii.
Bi.Jasmin alifafanua kuwa jamii hupata taarifa, elimu na uelewa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uwajibikaji wa viongozi wa Umma. “ katika muktadha huo vyombo vya habari vina nafasi kubwa na ya kipekee sana katika jamii yetu” alisema.
Katika hatua nyingine katibu huyo alifafanua kuwa ushirikiano wa Sekretarieti na vyombo vya habari nchini ni suala lisiloepukika kwani utasaidia kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma, Utaongeza uwajibikaji na uwazi katika utendaji wa shughuli za umma pamoja na kusaidia katika kukemea na kufichua vitendo visivyo na maadili kwa viongozi wa umma.
’’Maadili ya Viongozi wa Umma ni msingi muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji, uadilifu na utawala bora bila maadili imara jitihada zote za maendeleo ya taifa letu haziwezi kufikia malengo yaliyokusudiwa hivyo basi niwaombe tushirikine kwa pamoja kuhahikisha kuwa suala hili la kukuza na kuimarisha maadili linafanikiwa’’ alisema.
Akitoa neno la shukrani mmiliki wa Manyunyu media Bw. Benny Majata alisema kuwa kikao kazi hicho kimewajengea uwezo na uelewa mkubwa juu ya majukumu yanayotekelezwa na Taasisi hiyo
“Mimi kama mdau wa habari ninaahidi ushirikiano wa kina na Sekretarieti ya Maadili katika kuhakikisha kwamba malengo ya Taasisi na Serikalikwa ujumla yanatimia” alisema.
