RC MWANZA AWATAKA VIONGOZI MKOANI HUMO KUFANYA KAZI KWA UADILIFU
Katika kuboresha utendaji kazi na kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi, Viongozi na watumishi mkoani Mwanza wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili,weledi,uwajibkaji wa pamoja na uaminifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo wenye lengo la kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuimarisha imani ya wananchi kwa Viongozi wao umetolewa tarehe 26 Februari, 2026 jijini Mwanza na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Said Mtanda wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa Viongozi wa Mkoa huo yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa-Mwanza.
“Mafunzo haya ni nyenzo katika kuhakikisha kunakuwa na utamaduni wa uadilifu, hofu na haki katika kufanya maamuzi, kwani maadili ndio uti wa mgongo katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla,”alisema.
Mhe. Mtanda ameongeza kuwa Kiongozi muadilifu anatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwani zitasaidia katika kumuweka salama akiwa katika utumishi wake na ata akiwa amestaafu huku akiwaomba Viongozi hao kuendelea kujaza Tamko la Rasilimali na Madeni ambalo kwa sasa linafanyika kidijitali.
“Ndugu zangu tujifunze kuwajibika kwa mujibu wa sheria zinavyotaka,kwani hii itatuweka salama wakati tukiwa ofisini na ata tukishastaafu utumishi wetu na pia tujaze Tamko la Rasilimali na Madeni kwa uwazi, ukweli bila kuficha chochote hiko ni kitu muhimu sana,”alisema Mhe. Mtanda.
Awali akitoa neno la utangulizi Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa-Mwanza Bw. Godson Kweka amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi wa Umma mkoani humo kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, kuzingatia maadili, kuepuka mgongano wa maslahi na kuendelea kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa wakati kwani Mwanza ni kati ya Mkoa ambao Viongozi wake wanajitaidi katika kujaza fomu hizo kwa wakati na kwa idadi kubwa.
“Tunasisitiza katika kufanya kazi kwa pamoja, kutanguliza mbele maslahi ya umma kwa ustawi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla na pia kuendelea kujaza Tamko la Rasilimali na Madeni kwa wakati maana lipo Kikatiba kwa Kiongozi wa Umma kutamka mali zake,”alisema Bw. Kweka.
Mafunzo hayo yamewashirikisha Viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Mwanza ambao ni Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Wilaya, Madiwani, Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa pamoja na Makatibu Tawala.
