Rasimu ya mkataba wa huduma kwa mteja kujadiliwa.

Wadau mbalimbali kutoka Sekta mbalimbali nchini, wamekutana kujadili rasimu ya mkataba wa huduma kwa mteja wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tarehe 07 Novemba, 2022.
Akifungua Mkutano huo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa Sekretarieti imeona ni vyema kuwakutanisha wadau hao muhimu kushiriki katika kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali ya namna bora ya kuboresha utoaji huduma kwa wateja wao.
Mhe. Kamishna alifafanua kuwa mkataba wa huduma kwa mteja ni mwongozo unaoilazimisha Taasisi kutekeleza majukumu yake katika viwango vya juu vinavyokubalika. “Tumewaiteni leo ili kupata mapendekezo yenu ambayo yatakua ndio msingi wa mkataba huu” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Kamishna aliwasihi washiriki wa mkutano huo kutoa michango yao ya hali na mali ili kupata mkataba wa huduma kwa mteja ulio bora.” Ni matumaini yangu kuwa wajumbe wote mtashiriki kikamilifu katika kutoa maoni yatakayowezesha kupata mkataba wa huduma kwa mteja ulio bora, unaokidhi matakwa na matarajio ya wateja ambao ndio ninyi na wengine mnaowawakilisha hapa leo” alisema.
Rasimu hiyo ya mkataba wa huduma kwa mteja imeandaliwa na timu ya watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora.