Rais Samia afanya uteuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemteua Jaji mstaafu, Rose Teemba kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili kuanzia Aprili 24 Aprili, 2023.
Mhe. Rais alifanya uteuzi huo kwa mujibu wa kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 kinachoeleza kuwa Baraza la Maadili litakuwa na wajumbe watatu watakaoteuliwa na Rais, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa watu wenye wadhifa au wamewahi kuwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu.
Aidha, kifungu hicho cha 26(3) kinasema kuwa Rais, atateua mmojawapo wa Wajumbe wa Baraza kuwa Mwenyekiti.
Kazi kubwa ya Baraza la Maadili ni kufanya uchunguzi wa kina wa malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya viongozi wa umma waliotajwa katika kifungu cha 4 cha Sheria hiyo.
Aidha, uchunguzi huo hutanguliwa na uchunguzi wa awali ambao kwa mujibu wa kifungu cha 18(2)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hufanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Jaji mstaafu Teemba anachukua nafasi ya Jaji mstaafu Ibrahim S. Mipawa aliyemaliza muda wake, akiongoza Baraza hilo tangu Agosti 16, 2019 alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Jaji mstaafu Teemba anakuwa Mwenyekiti wa tano wa Baraza la Maadili toka kuanzishwa kwake akitanguliwa na Jaji mstaafu Damian Lubuva, Jaji mstaafu Hamis Msumi, Jaji mstaafu Januari Msofe na Jaji mstaafu Ibrahim Mipawa.