JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

BARAZA LA MAADILI LAHITIMISHA KUSIKILIZA TUHUMA ZINAZOMKABILI PROF. SEDOYEKA
17 Oct, 2024
BARAZA LA MAADILI LAHITIMISHA KUSIKILIZA TUHUMA ZINAZOMKABILI PROF. SEDOYEKA

 

Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma limehitimisha kikao chake cha siku mbili cha kusikiliza tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma zilizokuwa zikimkabili Mkuu wa chuo cha Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani  Sedoyeka.

Kikao hicho kilichohitimishwa tarehe 17.10.2024 kiliongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Rose Teemba akisaidiana na wajumbe wa Baraza Bw. Peter Ilomo na Bi Suzan Mlawi.

“Baraza litafanya hitimisho baada ya kusililiza pande zote mbili, ushauri utapelekwa kunako husika,” alisema Mhe. Teemba baada ya Prof. Sedoyeka kutoa utetezi wake.

Prof. Sedoyeka alikuwa akikabiliwa na mashtaka manne anayodaiwa kutenda wakati akitimiza majukumu yake ya uongozi.

Mashtaka hayo ni kumpandisha cheo Bw. Hakimu Ndatama kutoka Afisa Rasilimaliwatu daraja la II kuwa Mkuu wa sehemu ya Rasilimaliwatu bila kuwa na sifa, kuwa na mgongano wa maslahi kwa kufanya uamuzi wa kumnufaisha Bw. Ndatama, kuingilia mchakato wa zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza katika kampasi ya Babati kwa kuifuta bila kufuata utaratibu na kufanya uhamisho wa ndani wa Afisa Ugavi kutoka kitengo cha Ununuzi na Ugavi kwenda Idara ya Maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi.

Akiwasilisha mashtaka mbele ya Baraza tarehe 16 Oktoba, 2024 Wakili Mkuu wa Serikali Bi Emma Gelani alilieleza Baraza kuwa mlalamikiwa anakabiliwa na mashtaka manne na ameshindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) 6(1)(c) na 12(1)(c) vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Mlalamikiwa wakati akitekeleza majukumu yake ya uongozi pasipo kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma alimpandisha cheo Bw. Hakimu Ndatama kutoka Afisa Rasilimali II kuwa Mkuu wa sehemu ya Rasilimaliwatu kabla ya kukamilika kwa uhamisho wa mtumishi.”

Hata hivyo, Prof. Sedoyeka alikana tuhuma zote zilizowasilishwa mbele ya Baraza.

Bw. Ndatama ambaye ni mmoja kati ya mashahidi sita waliotoa ushaidi mbele ya Baraza alikiri kuwa tarehe 13.5.2023 alipandishwa cheo kutoka Afisa Rasilimaliwatu II kuwa Mkuu wa sehemu wa IAA kabla ya taratibu za uhamisho kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii hazijakamilika.

Akitoa utetezi wake mbele ya Baraza kuhusu tuhuma hiyo, Prof. Sedoyeka alisema, “Sikuwa na mamlaka ya kumpandisha cheo Bw. Hakimu, isipokuwa nilimteua na kumpangia majukumu. Nilimteua kwa nia njema ya kuongeza ufanisi, kwa maelezo hayo, naomba Baraza lako lifute shtaka hili kwasababu nilitekeleza kwa nia njema.”

Kuhusu lalamiko la kufanya uamuzi wa kumnufaisha Bw. Hakimu, Mkuu huyo wa chuo alilieleza Baraza kuwa hakuhusika na mchakato wa kumuombea uhamisho Afisa huyo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda IAA.

“Mimi sikuhusika kwa namna yoyote ile, kuomba Bw. Hakimu kuja IAA alipata barua tarehe 9.3.2023 wakati mimi nililipoti IAA tarehe 13.3.2023, hivyo, sikusaini barua yake ya kuomba ahamie wala kukumbushia,” alieleza.

Kuhusu kuingilia zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza na kuifuta kinyume kifungu cha 59(2) cha Sheriai ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, Mkuu huyo wa chuo alilieleza Baraza kuwa Taasisi yake ilipohitaji viti katika kampasi ya Babati, alielekeza iundwe kamati kutembelea maeneo tofauti nchini kuangalia mzabuni mwenye uwezo.

“Nilielekeza Kitengo cha Manunuzi kumhusisha mzabuni Timber and Hardware Ltd na kamati ilikuwa na mapendekezo yake,” alisema na kuongeza kuwa, “Baada ya mchakato kufanyika, nilipitia nyaraka za mchakato .wa ununuzi na kugundua kuwa kuna wazabuni wawili walikuwa na bei ndogo hawakushinda kwa madai kuwa bidhaa zao hazikufikia viwango, watu hawa walishinda zabuni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini kwetu hawakufikia viwango.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, taarifa ya ukaguzi ya vifaa husika haikuwa na maelezo ya kitaalam kukataa wazabuni waliokuwa na bei nafuu.

“Kwangu mimi hii ni dosari, nilikuwa kwenye mtanziko, nikaamua kufanya kikao na mwenyekiti wa Bodi ya zabuni tukakubaliana kuwa hata tukitangaza zabuni upya kwa kuwa nyaraka ni zilezile, hakuna jinsi atashinda Jaffery ING Sign Ltd aliyekuwa na bei kubwa.”

Katika mchakato huo wa ununuzi wa viti na meza, jumla ya kampuni nne zilijotokeza ikiwemo Jaffery ING Sain Ltd iliyopata zabuni kwa shilingi 1,144,057,200/, Timber and Hardware Ltd 1,013,974,000.03, Vadeck Investment Company Ltd iliyoomba zabuni kwa shilingi 762,625,003/= na kampuni ya Mult Cable Ltd kwa gharama ya shilingi 1,163,527,200.03.

Prof. Sedoyeka alifuta zabuni kwa madai kuwa gharama ilikuwa kubwa kuliko bajeti ya taasisi ya shilingi bilioni 1.274 Mchakato huo uliositishwa Juni, 2023, hadi sasa hivi bado haujakamilika.

Shahidi wa kwanza katika lalamiko hilo Bw. Ramadhani Mwanang’waka ambaye ni Afisa wa Sekretarieti ya Maadili alisema kuwa “baada ya kupitia nyaraka za zabuni tulibaini kuwa sababu za kusitisha zabuni hazikuwa miongoni mwa sababu zilizohainishwa kisheria.”

Kuhusu uhamisho wa ndani wa Bw. Robert Mwitango Afisa Ugavi kutoka kitengo cha Ununuzi na Ugavi kwenda Idara ya Maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi, aliliambia Baraza kuwa, “Mimi ninayo mamlaka kumpangia shughuli nyingine mtumishi na uhamisho huu ulikuwa na nia njema kwa maslahi ya Taasisi.”

“Kitengo cha Unununzi kilikuwa na watumishi 10, Idara ya Maktaba ilikuwa na upungufu wa watumishi na walitaka kufanya ununuzi mkubwa wa vitabu, kutokana na uhaba mkubwa wa rasilimaliwatu katika Maktaba, niliona kuhamisha mtumishi ni suala la kawaida katika taasisi,” alilieleza Baraza.

Bw. Robert aliyefika mbele ya Baraza kutoa ushahidi, alikiri kuhamishiwa Idara ya Maktaba kwa barua ya tarehe 6.10.2023 ambayo haikubainisha majukumu ya kazi.

“Nililipoti Maktaba nakupangiwa kukaa mapokezi kukagua wanafunzi wanaoingia na kutoka ndani ya Maktaba.”

Bw. Robert ni Afisa ugavi daraja la I ambaye ni Certified Procurement and Supply Professional (CPSP).

Wakili Gelani alilieleza Baraza kuwa .“uhamisho huu ulifanyika bila kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Utumishi wa Umma kinachowataka wakuu wa Taasisi kusimamia na kuhakikisha watumishi wanakuwa katika taaluma zao.” “kitendo hiki ni kinyume na Kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Maadili.”.

Wakati akimsomea mashtaka mlalamikiwa, Bi. Gelani aliliambia Baraza kuwa, “Malalamiko dhidi ya Prof. Sedoyeka ni kinyume na kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili kinachomtaka kiongozi wa umma kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria za nchi,”alisema.

 

 

 

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >