PAC YAIAGIZA TBA KUKAMILISHA JENGO LA MAADILI KWA WAKATI.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa wakati.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Naghenjwa Kaboyoka alitoa agizo hilo wakati wa ziara ya wajumbe hao waliyofanya katika mradi wa jengo la Sekreterieti ya Maadili linalojengwa katika mtaa wa Kilimani jijini Dodoma. Ziara hiyo ilifanyika tarehe 13 Machi, 2024.
”Mradi huu umekua na nyongeza ya mkataba kwa muda wa miezi 17 jambo ambalo linaweza likaipa Serikali yetu hasara kwa hiyo niwaombe wenzetu wa TBA mkamilishe mradi huu kwa wakati kulingana na mkataba wa sasa unavyotaka,” alisema.
Kwa mujibu wa mkataba wa awali, jengo hilo lilitakiwa kukamilika Desemba 15, 2022 ambao umeongezwa hadi tarehe 3 Mei, 2024.
Wajumbe wa kamati wameeleza kuwa kutokamilika kwa wakati kwa mradi huo kunaisababishia hasara serikali kwa kuendelea kulipia Sekretarieti ya Maadili gharama za pango ambazo zingetumika kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Bw. John Kaole, Katibu Usimamizi wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ameiambia Kamati ya Bunge kuwa ujenzi wa jengo hilo utagharimu kiasi cha shilingi 9,064,275,060.04.
Alieleza kuwa ujenzi huo, ulianza 14 Juni,2019 na mpaka sasa umefikia asilimia 95%.
Ziara hiyo ilijumuisha wajumbe wa Kamati ya Bunge, wajumbe kutoka Sekretarieti ya Maadili, Wajumbe kutoka Wakala wa majengo Tanzania pamoja na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.