Orodha ya makosa ya ukiukwaji wa maadili kuhuishwa

Orodha ya makosa ya ukiukwaji wa maadili kuhuishwa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza mchakato wa kufanya marekebisho ya makosa ya ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995, kwa lengo la kuboresha kifungu cha 19 (1) cha sharia hiyo chenye orodha ya makosa ya ukiukwaji wa maadili kwa Viongozi wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma.
Akifungua kikao kazi hicho Katibu Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Waziri Kipacha, alisema kuwa, Sekretarieti ya Maadili imechukua uamuzi huo wa kupitia upya na kuhuisha viambata vya makosa hayo ya ukiukwaji wa maadili, kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Maadili pamoja na Kanuni zake ambayo imeongeza wigo wa makosa ya sheria.
“Tukae tujadili makosa haya, na kama kwa mujibu wa mabadiliko ya Sheria yaliyofanyika tukaona kuna haja ya kuongeza makosa yaliyoongezwa kupitia Kanuni mbalimbali zilizofanyiwa marekebisho tuongeze, lakini pia, kama tutaona kuna haja ya kuboresha, tuboreshe, ili Taasisi yetu iweze kusimamia haki kwa Viongozi tunaowasimamia” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Kipacha alieleza kuwa, Sheria ya Maadili imeeleza kuwa, uchunguzi unaotakiwa kufanywa na Sekretarieti ya Maadili ni Uchunguzi wa awali utakaopelekwa katika Baraza la maadili kwa ajili ya kufanya Uchunguzi wa kina hivyo ni wajibu wa Taasisi kufanya uchunguzi huo kwa umakini wa hali ya juu na kujiridhisha wazi ni kosa gani la kimaadili ambalo kiongozi husika amekiuka.
“Taasisi hii, inawachunguza Viongozi wenye hadhi kubwa, kwa hiyo ni dhahiri kuwa, tunapaswa kutekeleza kazi hiyo ya uchunguzi kwa uadilifu na uweledi mkubwa, ili kulinda heshima na hadhi za viongozi hao” alisema.
Aidha, Bw. Kipacha, alisisitiza umuhimu wa kikao kazi hicho kuwa, kina kazi ya kuhakikisha kwamba kinatoa mapendekezo yatakayoiwezesha Taasisi kutekeleza majukumu yake vizuri ya kuisimamia Sheria.
“Naamini kuwa, baada ya kikao kazi hiki, tutatoka na viambata vya makosa ya ukiukwaji wa Maadili ambavyo vitatusaidia katika kukamilisha na kupata ushahidi wa kutosha ili tuweze kupeleka mashauri yetu katika Baraza la Maadili, ambalo ndilo lenye mamlaka ya kutoa mapendekezo kwa mamlaka ya nidhamu ya Kiongozi husika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu”, alisema.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Kitengo cha huduma za Sheria, Bi. Emma Gelani, alieleza kuwa, kikao kazi hicho cha siku tatu kitafanya kazi ya kipitia upya na kuhuisha viambata vya makosa ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili, kwa lengo la kusaidia na kuwezesha kazi ya kiuchunguzi kuwa rahisi katika utekelezaji wa kazi zao, kama za kukusanya ushahidi utakaopelekea kuwa na matokeo mazuri mbele ya Baraza la Maadili.
Makosa ya ukiukwaji wa Maadili yameainishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yam waka 1977, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Kanuni zake.