MWANGESI: WAHARIRI TUMIENI KALAMU ZENU KUANDIKA UMHIMU WA MAADILI KWA VIONGOZI

Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kuandika umuhimu wa maadili kwa viongozi wa umma ili kusaidia kukuza uadilifu wao katika utendaji wa kuwatumikia Wananchi na kuleta maendeleo.
Wito huo, umetolewa na Kamishna wa Maadili Mheshimiwa Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya Habari nchini uliolenga kuwajengea uelewa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995 pamoja na mafanikio ya miaka mitano. uliofanyika Leo Mei,24, 2024 katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania mkoani Dar es Salaam.
“Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma peke yake haiwezi kutoa elimu ya uadilifu bila msaada wa wadau wengine mkiwemo nyie wahariri wa vyombo vya Habari tunawategemea sana” alisema Jaji Mwangesi.
Mhe. Jaji (Mst) Mwangesi aliwasisitiza Wahariri Kwenda kuandika makala za kichambuzi, kufanya mahojiano na wataalamu wa masuala ya maadili pamoja na wananchi, kufanya uchunguzi wa kina na kuandika ripoti za kuchambua tabia na maadili ya Viongozi kwa kina.
Aidha, Kamishna Mwangesi amelipongeza Jukwaa la Wahariri kwa ushirikiano wanaoutoa kila siku kwa Sekretarieti ya Maadili kwa kuendelea kuchapisha habari zinazohusu uadilifu wa viongozi wa umma nchini.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Bw. Sadick Yassin ameiomba Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa wananchi ili waijue vizuri ofisi pamoja na majukumu yake na kuongeza wigo wa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Ikiwezekana mutumie mitandao ya kijamii, kubandika ata matangazo kwenye nguzo na mbao mbalimbali ili wananchi waijue vizuri ofisi”alisema
Akielezea mafanikio ya Sekretarieti, Mkurugenzi wa ufuatiliaji na mipango Bw. Omary Juma alisema kwa kipindi cha miaka 2 iliyopita wastani wa uwasilishaji malalamiko kwa mwezi umeongezeka kutoka malalamiko 16 mwaka 2021/22 hadi malalamiko 18 kwa mwaka 2022/23.
"Ongezeko hilo ni sawa na 13% hali hii inaonyesha vyombo vya Habari nchini vimekuwa na mchango mkubwa wa kutoa elimu na kupelekea wananchi kupata uelewa juu ukiukwaji wa maadili.