Mwangesi: Maadili yanapaswa kuanza na sisi wenyewe.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Mbeya wametakiwa kuzingatia maadili wao wenyewe kabla ya kuwahimiza wengine kufanya hivyo.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi wakati akizungumza na Watumishi hao jijini Mbeya alipofanya ziara ya siku mbili mkoani Mbeya ikiwa ni mara yake ya kwanza kutembelea Ofisi hizo tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwezi Desemba, 2020.
“Tuna wajibu mkubwa wa kuitetea taasisi yetu kwa kuzingatia viwango vya juu vya maadili wakati tunapotekeleza majukumu yetu kabla ya kuwahimiza wengine kufanya hivyo.Itakuwa ni aibu ikiwa wewe msimamizi wa maadili ukikiuka maadili.Nawasihi kufanya vile jamii na Serikali inavyotarajia tuyafanye”alifafanua Mhe. Mwangesi.
Kuhusu utunzaji wa siri, Mhe. Mwangesi alisema kuwa taasisi hii inatunza taarifa nyeti za viongozi wa umma hivyo hategemei kuona taarifa hizo zinazagaa mitaani na kuwasihi watumishi hao kujisahihisha kwa yale ambayo wanahisi kuwa hayapo sawa.
Akijibu changamoto iliyowasilishwa na Katibu Msaidizi wa Kanda hiyo Bw. Paul Kanoni kuhusu ufinyu wa bajeti unaokwamisha utekelezwaji wa mpango kazi wao, Mhe. Mwangesi alisema kuwa changamoto hiyo ni ya kitaifa na kwamba inatokana na Serikali kuelekeza fedha nyingi katika ukamilishwaji wa miradi mikubwa ya taifa ya maendeleo na kuwaasa kuendelea kutumia vizuri fedha inayopatikana huku wao kama viongozi wa taasisi wakiendelea kuziomba mamlaka husika kuiongezea taasisi hiyo ukomo wa bajeti yake.
Awali, Mhe. Mwangesi alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ofisini kwake ambapo katika mazungumzo yao walikubaliana kupitia Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyopo mkoani humo kuendelea kushirikiana katika kukuza uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma katika mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Homera alimweleza Kamishna wa Maadili kuwa amelazimika kuitisha Semina ya Maadili kwa viongozi wote wa taasisi za serikali katika mkoa huo kwa sababu mkoa wa Mbeya una mambo mengi ikiwemo changamoto za kimaadili.
Kwa mujibu wa Mhe. Homera, mkoa huo unatekeleza miradi mingi ya serikali na wakati mwingine inaibuka migongano ya kimaslahi kwa baadhi ya viongozi wa umma wanaosimamia miradi hiyo bila ya wao wenyewe kujua hivyo ni matarajio yake kuwa elimu ya maadili itakapotolewa kwa viongozi hao itasaidia kuondoa migongano hiyo.
Mhe. Mwangesi yupo katika ziara ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo kesho tarehe 23 Septemba, 2021 anatarajia kuzungumza pamoja na kutoa elimu kwa viongozi wote wa mkoa wa Mbeya pamoja na viongozi wa taasisi zote za serikali zilizopo mkoani humo.