Muongozo wa Uhakiki wahuishwa.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma kuhuisha mwongozo wa uhakiki waRasilimali , Maslahi na Madeni ya Viongozi wa Umma katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Point Zone Jijin Arusha tarehe 30 Mei 2022.
Akifungua kikao kazi hicho Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa ipo haja ya mwongozo wa uhakiki kuhuishwa kutokana na uhitaji uliosababishwa na maendeleo yaliyoletwa na matumizi mapana ya TEHAMA na tabia ya baadhi ya Viongozi kutokua waadilifu.
Mhe. Kamishna aliongeza kuwa Lengo la kuhuisha mwongozo huo sio tu kuwajengea uwezo wa uhakiki mali lakini kunawawezesha kuzingatia Maadili ya uhakiki, Sheria ,Kanuni na taratibu zenye kulinda heshima ya watumishi na Sekretarieti kwa ujumla.
“Kazi yoyote nzuri inategemea weledi wa watendaji hivyo basi ili kufanikisha hilo mwongozo wa uhakiki pia umeainisha maadili ya uhakiki na wahakiki wakati wa zoezi husika”alisema Mhe. Kamishna
Pamoja na hayo katika hotuba yake Mhe. Kamishna alifafanua kwamba kutokana na marekebisho katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyofanyika mwaka 2006 Sekretareti ya Maadili ilianza zoezi la uhakiki wa rasilimali na madeni ili kujiridhisha na uhalisia wa uhalali wa mali alizotamka kiongozi kama zinatokana na vyanzo vyake halali vya mapato. Pia kuhakikisha kama anashughulika na rasilimali na maslahi hayo bila kuleta mgongano wa maslahi.
Mhe. Kamishna aliendelea kufafanua kuwa lengo la msingi la uhakiki limekua ni pamoja na kuthibitisha kama Tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni linalotolewa na Kiongozi wa Umma ni sahihi; kujiridhisha kama thamani ya mali iliyotajwa katika tamko la Kiongozi inawiana au ndiyo thamani halisi ya mali husika.
Sambamba na hayo ni kutambua kama kuna rasilimali nyinginezo ambazo kwa makusudi hazikutamkwa; kutambua kama Kiongozi ana vyanzo Vingine vya mapato ambavyo hakuvitamka kwenye tamko lake na kutambua kama kuna rasilimali, maslahi au shughuli zinazo mwingiza Kiongozi kwenye Mgongano wa Maslahi.
Mhe. Kamishna alisisitiza kuwa Sheria inawataka Viongozi wa Umma kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, huruma ,umakini kujizuia na tamaa na kuridhika,kutoa tamko la Rasilimali , Maslahi na Madeni, kutopendelea, kujizuia na mazingira yatakayosababisha mgongano wa Maslahi, kutangaza hadharani maslahi ya fedha na kutoa Tamko la Kimaslahi kuhusu mikataba yao au na Serikali
Sekretarieti iliandaa mwongozo wa uhakiki ambao umekua ukiboreshwa kuendana na wakati. Mwongozo huu kwa mara ya mwisho ulirekebishwa mwaka 2021 ili kuongeza suala la uhakiki wa mgongano wa maslahi kutokana na kutungwa kwa Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi za mwaka 2020.