Mkuu wa Mkoa wa Sindida awataka watumishi wa umma kuzingatia uadilifu wanapotekeleza majukumu yao.

Watumishi wa umma mkoani Singida wamewatakiwa kuzingatia suala zima la uadilifu wanapotekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa kuzingatia haki kwa kila mmoja.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Bi. Halima Dendego ametoa wito huo katika Kongamano la Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, lililofanyika tarehe 10 Desemba,2024 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
"Siku hii ina maana kubwa sana kwetu. Sisi watumishi wa umma tunatakiwa kujitafakari kwa namna tunavyotekeleza wajibu wetu katika kutoa huduma kwa umma kuwa tunatakiwa kufanya hivyo kwa kuzingatia haki za binadamu, kuwa waadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.’’alisema.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Kongamano hilo ni muhimu kwa sababu linatoa nafasi kwa viongozi na watumishi wa umma kujitathmini na pia kutathmini mchango wao katika kufikia lengo la Serikali la kikatiba la kuleta ustawi kwa wananchi wake.
Kongamano hilo lilijumuisha watumishi wa umma wa Sekretarieti ya Mkoa wa Singida, halmashauri ya Wilaya ya Sindida pamoja na taasisi nyingine za umma mkoani humo.
‘’Ni muhimu kutumia Kongamano hili kujitathmini na pia kufanya kazi kwa kujielekeza kutoa huduma nzuri kwa wananchi, kuzingatia uadilifu wa hali ya juu na kutenda matendo mema yenye kuleta faraja kwa wananchi wetu,’’ alisisitiza Bi. Dendego.
Awali akitoa neno la utangulizi katika Kongamano hilo, Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati, Dodoma Bi. Jasmin Awadhi amesema kuwa Kongamano hilo linatokana na matukio mawili muhimu Duniani.
‘’Maadhimisho haya ni muunganiko wa matukio mawili ya Kimataifa. Kwanza ni Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa ambayo Mkataba wake ulisainiwa mjini Merida Mexico tarehe 9 Desemba, 2003 ambayo huitwa siku ya Maadili na siku ya pili ni Siku ya Haki za Binadamu iliyotokana na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu uliosainiwa tarehe 10. 12.1948,” alisema.
Kwakuwa nchi yetu uadhimisha siku ya Uhuru tarehe 9 kila Desemba, Serikali iliamua kusongeza mbele Siku ya Maadili na kuiadhimisha tarehe 10 ambayo pia ni Siku ya Haki iza Binadamu. Tangu mwaka 2016, Serikali iliunganisha siku hizo mbili na kuziita Siku ya Maadili na Haki za Binadamu.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka 2024 ilikuwa “Tumia haki yako ya kidemokrasia chagua Viongozi waadilifu na wanaozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa maendeleo ya Taifa.”