JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

MKURUGENZI PSSSF AFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA MAADILI.
27 Oct, 2023
MKURUGENZI PSSSF AFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA MAADILI.

Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA katika Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Gilbert William Chawe tarehe 16 Septemba, 2022 alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ikiwa ni pamoja nakukopa kiasi cha shilingi 200,765,838.00 kinyume na utaratibu wa Mfuko.

Akisoma mashtaka hayo Wakili wa Serikali Bw.Hassan Mayunga alisema kuwa Bw. Chawe alitumia fedha za umma katika mfuko wa PSSSF kiasi cha shilingi 135,630,448.00/=, bila kufuata utaratibu, kwa kuzikopa na kununua gari binafsi hali akijua kuwa fedha hizo hazikutengwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021.

Aidha, wakili Mayunga aliongeza kuwa katika shitaka la pili, mlalamikiwa akitekeleza majukumu yake ya kikazi kati ya mwaka 2020 na 2021 alipokea na kutumia bila kufuata utaratibu fedha za umma kutoka PSSSF kiasi cha shilingi 65,133,390.00 kwa ajili ya kulipia kodi ya ununuzi wa gari binafsi ambao haukufuata utaratibu.

“Kitendo hicho Mwenyekiti ni kinyume cha kifungu cha 6(1)(a),(b) na (f) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 3(2)(a) na (e) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi na Kanuni 7(d) na (e) ya Kanuni za Ahadi ya Uadilifu,” alisema.

Shtaka la tatu alilosomewa ni kupokea fedha kiasi cha shilingi 65, 133,390.00 kutoka PSSSF kwa ajili ya kulipia kodi ya ununuzi wa gari binafsi, lakini kiasi hicho kilitumika kinyume na utaratibu na pia hakikutumika kama ilivyokusudiwa.

Mlalamikiwa amekana malalamiko yote matatu.

Ilidaiwa mbele ya Baraza kuwa mlalamikiwa alipata mkopo huo kinyume na sera ya mikopo ya PSSSF na kuwa mkopo huo haukupita kwenye kamati ya mikopo ya taasisi.

Upande wa mlalamikaji uliliambia Baraza kuwa, “Sera ya mikopo ya PSSSF ya tarehe 1/11/2018 kipengele cha 4.2.(b)(viii) kinasema kuwa mfuko utalipa asilimia mia moja ya kodi kwa Mkurugenzi mkuu na wakurugenzi wengine kwa gari jipya, lakini gari alilonunua mlalamikiwa halikuwa jipya bali ni garichakavu.”

Aidha upande wa mlalamikaji uliwasilisha vielelezo mbalimbali ikiwemo mkataba wa mkopo uliosainiwa Aprili 24, 2021, orodha ya wanufaika wa mkopo na hati ya malipo ya tarehe 29 Aprili, 2021.

Hata hivyo, ushahidi kutoka Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) unaonyesha kuwa gari alilonunua Bw. Chawe lenye nambari za usajili T607DTQ lilisajiliwa kwa mara ya kwanza na mamlaka hiyo tarehe 12/6/2020 na mmiliki wake wa kwanza ni Bw. Kipemka Msemembo Musa.

“Mnamo tarehe 4 Mei, 2021 umiliki wa gari hilo ulihamia kwa Bw. Chawe kutoka kwa Salim Cars wa Dar es Salaam. Salim Cars alilinunua kutoka kwa Jaji Musa wakati gari hilo lilisha lipiwa kodi na Serikali,” ulieleza upande wa malalamiko.

Serikali ilinunua gari hilo na kumpa Jaji Musa kama stahiki yake alipostaafu.

Mlalamikiwa amekiri mbele ya Baraza kuwa mmiliki wa kwanza wa gari hilo ni Jaji Musa.

“Ni kweli gari hilo alipewa Jaji Musa kama stahiki yake, lakini aliliacha Toyota kwa lengo la kutafuta mnunuzi mwingine,” alisema Bw. Chawe.

Alipoulizwa kama Salim Cars anayedaiwa kulinunua kutoka kwa Jaji Musa alimuonyesha hati za malipo ya kodi, mlalamikiwa ameshindwa kulithibitishia Baraza.

“Mfuko wa PSSSF ulimlipa fedha za kodi Salim Cars, sio mimi, malipo haya yalilipwa baada ya kujiridhisha na kiasi cha kodi kilichotakiwa kulipwa,’ alisema.

Hata hivyo mlalamikiwa alipoulizwa mbele ya Baraza kama kiasi cha shilingi milioni 13.6 ambayo ni asilimia 10 ya Tsh 135 milioni iliyotakiwa kulipwa TRA kama gharama ya uhamisho wa umiliki wa gari ililipwa ameshindwa kulithibitishia Baraza malipo hayo.

Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lililokuwa chini ya Mwenyekiti wake Jaji (Mst.) Ibrahim Mipawa limehitimisha vikao vyake vya uchunguzi vilivyoanza Septemba 6 kwa kusikiliza malalamiko tisa (9) ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Waliofikishwa mbele ya Baraza ni pamoja na Bw. Geofrey Chibulunje, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Hoseah Kashimba Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bi Beatrice Lupi, Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF, Bw. Ernest Khisombi, Mkurugenzi wa Ugavi na Ununuzi wa PSSSF na Bw. Peter Martin Sulle, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu.

Wengine ni Bi. Kapwete Leah John, Mkurugenzi wa sheria wa EWURA, Dkt. Ayoub Chacha Rioba, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Jerome Philip Kamwela, Mkurugenzi wa Tathimini na Ufuatiliaji wa TACAIDS na Bw. Gilbert William Chawe, Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA wa PSSSF.

Vikao vya Baraza la maadili ya viongozi wa Umma ni utekelezaji wa matakwa ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kuhusu kusimamia tabia na mwenendo wa viongozi wa umma waliotajwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >