JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Mhe. Mnyema: Zingatieni Misingi ya Maadili.
29 Feb, 2024
Mhe. Mnyema: Zingatieni Misingi ya Maadili.

Viongozi wa Umma  wameaswa kuzingatia misingi ya Maadili  ya Viongozi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuleta mchango wenye tija kwa serikali na wananchi kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhe. Pili Mnyema alipofungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi  wa Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Mnyema alisema kuwa  ipo misingi ya Maadili inayomuongoza  kiongozi yeyote namna anavyopaswa kutenda na kuenenda wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku misingi hiyo ni pamoja na Uadlifu, Uwazi, Uaminifu na ukweli, kuheshimu Sheria, Uwajibikaji, Haki na Kutopendelea, Kujiepusha na Mgongano wa Maslahi na mingine mingi.  

Mhe. Myema alieleza kuwa Dira ya Taifa  hususan kipengele cha utawala bora inasisitiza  kuwa  ifikapo    mwaka 2025 uadilifu uwe  sehemu ya utamaduni wa jamii ya Tanzania.” Kila wakati tumemsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili hivyo sisi kama viongozi ni lazima tutii”

“Niwaase Viongozi wenzangu tuache mienendo isiyofaa  mfano matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, ubadhilifu wa mali za umma ,kuomba na kupokea rushwa ama zawadi, kujilimbikizia mali na mengineyo yanayofanana na hayo na hii itatufanya kuwa waadilifu ili tuweze kwenda sawa na dira inayotuongoza” alisema.

Aidha Mhe. Myema  alitumia wasaa huo  kuwakumbusha viongozi hao  kuhusu  maelekezo mbalimbali ya Serikali  yanayohusu maadili na utawala Bora  kwamba kila kiongozi anapaswa kutanguliza maslah ya Taifa mbele badala ya  maslah yake binafsi, kiongozi anapaswa kushiriki katika kuimarisha utawala Bora nchini ili kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya Taifa badala ya kuviachia vyombo vinavyosimamia Utawala Bora, Kila kiongozi awe mzalendo katika kusimamia miradi ya maendeleo ya Nchi na mengine mengi.

Awali  akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji Maadili , Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Salvatory Kilasara alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili imeandaa mafunzo hayo kwa Viongozi husika lengo likiwa ni kuwambusha juu ya dhana nzima ya maadili.

“Tunafahamu kuwa nyote hapa mna uelewa juu ya dhana nzima ya Maadili lakini binadamu tumeumbiwa kusahau hivyo  sisi kama Taasisi inayosimamia maadili kwa Viongozi wa Umma ni jukumu letu kutoa elimu hii mara kwa mara  hivyo tumekuja kuwakumbusha kufuata  sheria ,kanuni na taratibu za utumishi wa Umma mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku’’ alisema 

Bw, Kilasara alitumia fursa hiyo kuwaasa Viongozi hao kuwa mfano wa kuigwa kwa kutenda yale wanayohubiri kwa watumishi walio chini yao kwa kutenda yaliyo mema mfano matumizi na usimamizi mzuri wa rasilimali za nchi, matumizi ya lugha ya staha nk. Ili kujenga Imani kwa watumishi walio chini yao na jamii kwa ujumla.

“Viongozi wenzangu huwezi kuwa jasiri wa kusimamia maadili kwa  watumishi walio chini yako kama wewe sio muadilifu kama binadamu lazima uone haya, hivyo tuishi yale tunayoyahubiri” alisema

Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ya siku moja ambazo ni pamoja na mada kuhusu Mgongano wa Maslahi, mada kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma, mada kuhusu Mgongano wa Maslahi, mada kuhusu Maadili na Uwajibikaji katika Utumishi wa Umma, na mada kuhusu  mifumo ya kudhibiti rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mgongano wa maslahi.

 

 

 

 

 

 

 

 

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >