Mahakimu wa Mahakama za Singida waaswa kuepuka kupokea zawadi
Mahakimu kutoka mahakama mbalimbali mkoani Singida wamesisitizwa kutokua na tabia ya kupokea zawadi mbalimbali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kujiepusha na mazingira yanayopelekea mgongano wa maslah, kuepuka mazingira ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa, uonevu, upendeleo na mengine yanayofanana na hayo.
Hayo yalielezwa na Kaimu Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya kati Dodoma Bw. Joshua Mwambande wakati akiwasilisha mada iliyohusu tamko la zawadi kwa viongozi wa Umma katika mafunzo ya maadili kwa waheshimiwa mahakimu hao. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Jalmin mkoani Singida tarehe 31 Mei, 2024
Bw. Mwambande alieleza kuwa endapo viongozi wa umma hususan mahakimu watakua na tabia ya kupokea zawadi kunaweza kuathiri utendaji kazi wao kwani zawadi hizo zinaweza kumshawishi kiongozi kufanya maamuzi yasiyo ya haki na kusababisha wananchi kukosa haki yao.
Kupokea zawadi kunaweza kumfanya kiongozi kufanya maamuzi ya upendeleo na kusababisha wananchi kukosa imani na viongozi wao na serikali kwa ujumla.
“Zawadi yoyote ina lengo ndani yake ,mtu anapokupa zawadi kuna kitu anakitegemea kwako, nyinyi ni mahakimu ndio watoa haki katika mahakama unapokua na tabia za kupokea zawadi bila kujua lengo lake unajiingiza katika mtego na kujikuta unafanya maamuzi ya upendeleo pindi mtu huyo anapohitaji huduma katika ofisi yako” alisema.
Katika hatua nyingine mahakimu hao walisisitizwa kuzingatia kiapo cha Ahadi ya Uadilifu ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa uwazi,uaminifu, uwajibikaji kwa maslahi mapana ya Taifa.
Aidha Viongozi wanaapa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu ili kuthibitisha dhamira yao ya kufuata maadili na kuwajibika ipasavyo katika utendaji wao wa kazi
Kiapo hicho ni ishara ya ahadi yao ya kuongoza kwa uwazi,uaminifu na kwa maslah ya Umma na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na makosa mengine ya kiuadilifu.
Aidha kiongozi akikiuka masharti ya hati ya Ahadi ya Uadilifu anakua amekiuka masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995
Aidha kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Singida Mhe. Allu Nzowa alisema kuwa mafunzo hayo ya maadili kwa mahakimu hao ni ya muhimu sana kwani yanawakumbusha misingi na miiko ya kazi yao
“kazi yetu ni kazi nyeti hivyo inapaswa kusimamiwa na watu wenye maadili ya hali ya juu hivyo sisi kama binadamu tumeumbiwa kusahau ni vyema tukakumbushana mara kwa mara hususan masuala ya maadili” alisema,
Mhe.Nzowa alitumia wasaa huo kuwaasa waheshimiwa mahakimu kuzingatia masuala mazima ya kutenda haki kutoa maamuzi bila upendeleo ili wananchi waweze kujenga Imani na mahakama zao na viongozi kwa ujumla.
“Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa mtu yeyote asiye na maadili anaweza kufanya kazi nyingine yoyote lakini sio ya uhakimu au ujaji, nah ii ni kutokana na unyeti wa kazi hii hivyo niwaombe mahakimu wenzangu tuwe waadilifu” alisema.
Katika mafunzo hayo mada mbili ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na mada kuhusu tamko la zawadi na mada kuhusu uzingatiaji wa kiapo cha ahadi ya uadilifu.