MADIWANI WA HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA WAMETAKIWA KUZINGATIA SHERIA YA MAADILI.

Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wametakiwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kujiepusha na vitendo vinavyopelekea kuwepo kwa Mgongano wa Masilahi katika utekelezaji wa Majukumu yao ya kila siku.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa Bwana Godson Kweka katika mafunzo ya Madiwani wa jiji hilo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na 13 ya mwaka 1995, Kanuni za Serikali za Mitaa za mwaka 2000 na mgongano wa Maslahi.
Aidha Bw. Kweka aliwataka Madiwani hao kuzingatia Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu walichoapa na wajibu wao katika kutekeleza kanuni za Serikali za Mitaa za mwaka 2000.
Akifungua mafunzo hayo Katibu Msaidizi anayeshughulikia Serikali za Mitaa Mkoa wa Mwanza Bibi Christina Bigambo alisema mafunzo hayo yanategemewa kuwa chachu ya ushirikiano kati ya Madiwani wa Jiji la Mwanza pamoja na Watendaji wa Jiji kwa nia ya kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi wa kazizao za kila siku.
Bibi Bigambo aliongeza kuwa Madiwani wanatakiwa kuzingatia Mada zote zitakazotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili ziwasaidie katika kuboresha utendaji wa kazi zao za kila siku kwa kufuata Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mafunzo hayo yalifungwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bibi Amina Makilagi ambapo aliwahimiza Madiwani hao kuzingatia mafunzo waliyoyapata katika kuwatumikia wananchi kwa weledi na uadilifu mkubwa.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalihudhuriwa na Madiwani 26 wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ambapo yalifanyika katika ukumbi wa Halmashaurihiyo jijini Mwanza.