MADIWANI WA HALMASHAURI YA CHAMWINO WASISITIZWA UWAJIBIKAJI WA PAMOJA.
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Chamwino, wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wengine wa halmashauri hiyo wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia uwajibikaji wa pamoja kwa kutimiza wajibu wao ili kuwaletea wananchi maendeleo,
Wito huo umetolewa na Bi. Jasmini Awadhi, Katibu Msaidizi Kanda ya Kati, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakati akitoa mafunzo maalumu kwa waheshimiwa madiwani na watalamu mbali mbali wa halmashauri hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Chamwino tarehe 8 Mei 2024.
Aidha Bi. Jasmini alifafanua kuwa, panapokuwepo na sintofahamu au kutoelewana kati waheshimiwa madiwani, wakuu wa Idara pamoja na watalamu waliopo kwenye vijiji na Kata mwisho wa siku anayeumia ni mwananchi na sio Kiongozi na kupelekea maendeleo kuchelewa kuwafikia wananchi kwa wakati.
"Waheshimiwa madiwani mnawajibu wa kuwasimamaia watumishi vizuri, sio kila mtumishi mnaona ni mwizi zingatieni ushauri wanaowapa watalamu, hivyo hivyo kwa watalamu sio kila ushauri unaotolewa na Diwani mnaona haufaii, hapa kuna madiwani wanataaluma kama zetu hivyo tukae kwa pamoja tujadili pamoja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii na Taaasisi mnayoingoza" Bi. Jasmini alisema.
Aidha, Bi. Jasmini amewakumbusha Viongozi kuzingatia maadili kwa wakati wote wanapokuwepo ofisini au nje ya ofisi, katika kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Umma ambapo amewataka madiwani hao pia kujiepusha na mgongano wa maslahi wakati wa utekelezaji wa miradi mbali mbali wanayoisimamia katika halmashauri zao.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Chamwino, Mhe. Edson Sweti ameishukuru Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kutoa elimu ya Maadili kwa madiwani pamoja na watalamu wengine wa halmashauri hiyo kwa masilahi ya wananchi wanaowaongoza, na ameongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo madiwani hao watafanya kazi kwa ushirikiano na uadilifu mkubwa kwa maslahi mapana ya umma na Taifa kwa ujumla.
Mafunzo hayo yaliwajumuisha waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Chamwino, Wakuu wa idara na vitengo pamoja na wataalamu mbalimbali wa halmashauri hiyo ambapo Mada mbili zilijadiliwa katika mafunzo hayo ambazo ni Mgongano wa Maslahi pamoja na Uwajibikaji wa pamoja.