MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI WAMETAKIWA KUZINGATIA MAADILI:

MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI WAMETAKIWA KUZINGATIA MAADILI:
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar wametakiwa kufanyakazi kwa Uadilifu na weledi mkubwa wnapotekeleza Majukumu yao kwa dhamana waliyopewa ili kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza pamoja na Serikali kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad alipokuwa akifungua mafunzo ya Maadili kwa Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika Chuo cha Polisi Zanzibar tarehe 29 Novemba 2023.
Kamishna Hamad katika hotuba yake ameeleza kuwa, jamii ikikosa imani na jeshi la polisi yaweza kupelekea amani ya nchi kutoweka na kusababisha migogoro nchini.
Aidha Kamishna Hamad alibainisha kuwa “kusimamia sharia bila uadilifu yaweza kusababisha machafuko katika nchi yetu” alisema.
Kamishana huyo pia alifafanua kuwa matendo yanayofanywa na jeshi la polisi katika kusimamia sharia ni lazima yawe ya mfano katika jamii na Serikali kwa ujmla.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Msaidizi Kanda Maalumu Bi Eliza Komba amewataka Maafisa hao kuwa mstari wa mbele katika kusimamia Maadili katika kutekeleza Majukumu yao kwa Uadilifu na weledi wa kiwango cha juu.
Bi Komba pia amewataka Maafsa hao kuyaishi yote yatakayofundishwa katika mafunzo hayo kupitia Mada mada mbali mbali zilizoandaliwa katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku.
Amefafanua kuwa miongoni mwa Mada zitakazojadiliwa ni pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mgongano wa Maslahi, Ahadi ya Uadilifu pamoja na Tamko la Raslimali na Madeni.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha Maafisa Waandamizi wa jeshi la Polisi kutoka Mikoa mitatu ya Unguja. Mkoa wa Mjini, Kaskazini Unguja na Mkoa wa Kusini Unguja.