MAAFISA WA JESHI LA POLISI WASISITIZWA KUZINGATIA KIAPO CHA UADILIFU.
Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini wametakiwa kuzingatia masharti ya kiapo cha Ahadi ya Uadilifu pamoja na sheria nyingine za nchi.
Wito huo umetolewa na Katibu Ukuzaji Maadili, Bw. Waziri Kipacha mara baada ya kuongoza kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa maafisa wandamizi 155 wa Jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo mbalimbali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma, tarehe 19 Februari, 2024 na kuhudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura.
Bw. Kipacha alieleza kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kilianzishwa ili kuongeza nguvu kwenye sheria, kanuni na maadili yaliyopo.
"Nimesikia wimbo wa maadili kutoka Jeshi la Polisi ni wimbo ambao umegusa mambo mengi yaliyopo kwenye kiapo mlicho apa muda mfupi uliopita, hivyo mambo hayo mkiyazingatia yatawasaidia katika utendaji wenu wa kazi wa kila siku kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni." Bw. Waziri Kipacha.
Bw. Kipacha aliwataka maafisa hao kutambua kuwa kiapo hicho ni dhamira ya ndani inayowaongoza kuwa waadilifu kwa kuzingatia misingi ya maadili na mikakati ya mapambano dhidi ya Rushwa.
"Sisi tunaimani na Jeshi la Polisi kuwa na nidhamu ya hali ya juu tunategemea maafisa mliokula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kuwa mfano kwa viongozi wote kwa kuzingatia uadilifu," alisema
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi DCP, David Misime ambaye ni miongoni mwa maafisa waliokula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu akiongea kwa niaba ya wenzake alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, kwa kufanikisha kuwapandisha vyeo maafisa hao na kumuhaidi kuwa vyeo hivyo vitawaongezea morali wa kazi na watavitumia kwa maendeleo ya Nchi na Jeshi la Polisi.