Maafisa Ununuzi na Ugavi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wajengewa uwezo
Maafisa Ununuzi na Ugavi kutoka Ofisi ya Rais ,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu na Kanda wamekutana katika kikao kazi chenye lengo la kuwajengea uwezo katika kurekodi, kutunza na kusimamia mali za Taasisi.
Kikao kazi hicho kimefanyika tarehe 27 Aprili, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) mkoani Singida na kufunguliwa na Kamishna wa Maadili nchini Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi.
Katika hotuba Jaji Mwangesi amewataka Maafisa hao kuhakikisha kuwa mifumo ya usimamizi wa mali inafanya kazi kwa ufanisi, kutoa ushauri unazingatia weledi na kuisaidia Taasisi kuepuka hasara kwa kuboresha matumizi ya rasilimali.
“Jukumu lenu halipo tu katika kutekeleza taratibu bali linaenda mbali zaidi hadi katika kutoa ushauri sahihi wa kitaalamu na unaozingatia sheria na kanuni katika usimamizi wa mali za umma,” alisema Mhe. Mwangesi.
Aidha Jaji Mwangesi ameongeza kuwa ni muhimu kwa Maafisa Ununuzi na Ugavi kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa sahihi ambazo ni muhimu katika muktadha wa ukaguzi kwani Taasisi nyingi utathiminiwa kupitia ukaguzi unaofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Moja ya matarajio ya Taasisi ni kupata hati safi na itambulike kuwa hati safi haipatikani kwa bahati mbaya bali inatokana na mifumo imara, nidhamu ya kazi na zaidi ya yote ni uwepo wa taarifa sahihi na zinazoaminika,” alisisitiza.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa iwapo taarifa zilizomo katika daftari la mali la Taasisi hazilingani na hali halisi au hazijakamilika na kuhuishwa kwa wakati uwezekano wa kupata hoja za ukaguzi huwa mkubwa na hoja hizo huathiri taswira ya Taasisi, huathiri utendaji wake pamoja na uaminifu mbele ya wadau wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Manunuzi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Kenedy Mwakalindile amesema kuwa kikao kazi hicho cha siku tatu kimelenga katika kutoa mafunzo na kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha kuwa wanakua na daftari lenye taarifa sahihi.
“Lengo la kukutana hapa ni kupitia daftari letu kwa pamoja na pia kulifanyia maboresho ili tuwe na daftari sahihi ambalo litatusaidia hapo mbeleni hasa kwenye ukaguzi kutoka nje,” alisema Bw. Mwakalindile.
Katika kikao kazi hicho mada mbalimbali zimetolewa ikiwemo namna ya matumizi ya Mfumo wa Kieletroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali (GAMIS).
