Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu yazinduliwa

Maadhimisho ya siku ya Maadili na haki za binadamu yalizinduliwa rasmi tarehe 03 Desemba, 2023 katika hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Zingatia Maadili, Utu, Uhuru, na Haki kwa watu wote kwa maendeleo endelevu”
Akizindua maadhimisho hayo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa maadhimisho hayo yana lengo la kuwakumbusha viongozi, watumishi na wananchi kwa ujumla wake juu ya dhana nzima ya kuwa na maadili, kukwepa vitendo vya rushwa, kuzingatia haki za binadamu, kufuata taratibu na kanuni mbalimbali za nchi jambo ambalo litaileta maendeleo katika jamii na Serikali kwa ujumla.
Mhe. Pindi aliendelea kusema kuwa jukumu la Serikali ni kuhakikisha kuwa inawaletea wananchi maendeleo hivyo usimamizi wa Maadili na mapambano dhidi ya rushwa na masuala ambayo lazima yatiliwe mkazo ili kuwa na viongozi, watumishi na jamii yenye madili na itakayokua mstari wa mbele katika kukwepa vitendo vya rushwa jambo ambalo litasaidia usimamizi na matumizi mazuri ya rasilimali za nchi.
“Serikali yetu chini ya Rais wetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan imekua ikipeleka fedha nyingi katika miradi mbalimbali lakini fedha hizo zimekua zikiishia katika mifuko ya watu wachache waliokosa maadili na kukwamisha juhudi za Serikali yetu, niwaase ndugu zangu tushiriki kwa pamoja kusimamia maadili na kupinga vitendo vya rushwa na tuiunge Serikali yetu mkono ili sote tufurahie rasilimali za nchi yetu” alisema.
Pamoja na hayo Mhe. Pindi alisema kuwa maadhimiso ya siku ya maadili na haki za binadamu yanapaswa kuwa endelevu ”Kuadhimisha siku hii kunatupa fursa ya kujitathmini ni wapi tulipotoka ni wapi tulipo na ni wapi tunaelekea katika suala zima la Maadili” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Pindi alitumia fursa hiyo kuwaasa baadhi ya watendaji wa serikali wasiofuata taratibu katika kutoa haki badala yake wanadai rushwa kwa njia mbalimbali jambo ambalo ni utomvu wa maadili “wapo baadhi ya watendaji wenzangu wanaotumia vyeo na madaraka yao vibaya kwa kudai rushwa kwa njia mbalimbali na kukiuka haki za binadamu kwa kutokutoa maamuzi ya haki, tunapaswa kujitafakari na kuzingatia viapo vyetu” alisema.
Shuhuli mbalimbali zitafanyika katika kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu kwa mwaka 2023 ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umaa kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini, jukwaa la wadau wa masuala ya rushwa, wiki ya kutoa huduma kwa jamii pamoja na kilele cha maadhimisho hayo tarehe 10 Desemba,2023.
Maadhimisho ya siku ya Maadili na haki za binadamu nchini, imetokana na siku mbili tofauti ambazo huadhimishwa kimataifa ambazo ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa pamoja na Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambapo kuanzia mwaka 2016 Serikali iliamua kuadhimisha siku hizi kwa pamoja hivyo mwaka huu ni wa saba (7) kwa maadhimisho haya kufanyika kwa pamoja.
Maadhimisho hayo huratibiwa na taasisi zinazosimamia utawala bora ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.