Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchini yazinduliwa rasmi

Maadhimisho ya siku ya Maadili na haki za binadamu nchini yamezinduliwa rasmi tarehe 06 Desemba, 2022 na kilele cha maadhimisho hayo ni tarehe 10 Desemba, 2022
Akizindua maadhimisho hayo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt Damas Ndumbaro (Mb) wakati akiongea na waandishi wa habari alisema kuwa jukumu kubwa la Serikali yetu ni kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo usimamizi wa maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, uwazi na mapambano dhidi ya rushwa ni suala endelevu kwa kuwa ni msingi wa utoaji wa huduma bora kwa umma.
Mhe. Ndumbaro alieleza kuwa ili Serikali iwahudumie wananchi walioiweka madarakani ipasavyo, haina budi kusimamia vyema matumizi ya rasilimali za nchi kwa maslahi mapana ya wananchi.” Tunapoadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu ni fursa nzuri ya kujitafakari tulikotoka, tulipo na tunapokwenda katika ujenzi wa Taifa letu” alisema.
Aidha Mhe. Ndumbaro aliongeza kuwauchumi wa nchi yetu umekuwa ukidumazawa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya Rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ambako huchangiwa na ukosefu wa maadili miongoni mwa watendaji kutoka sekta zote. “Serikali ya awamu ya tano kwa kutambua umuhimu wa mapambano dhidi ya vikwazo hivi imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa hivyo nitumie fursa hii kuwakumbusha wadau wote kuupitia vyema mkakati wa kitaifa dhidi ya rushwa na kujitathmini” alisema.
Pamoja na hayo Mhe. Ndumbaro alisema kuwa uwepo wa vitendo vya rushwa unaifanya Serikali kushindwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kuwahudumia wananchi ipasavyo jambo linanalofanya miradi ya maendeleo kushindwa kufanyika au kufanyika kwa kiwango cha chini kutokana na fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya serikali kuingia katika mifuko ya watu wachache.
Aidha katika maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu nchini kwa mwaka huu yatakua na shughuli mbalimbali kama wiki ya utoaji huduma kwa umma ambapo wananchi watapata fursa ya kukutana na watoa huduma mbalimbali katika viwanja vya Nyerere Square Jiji Dodoma .Kilele cha maadhimisho hayo ni tarehe 10 Desemba, 2022 na Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Prof. Hamis Juma.
Aidha Kauli mbiu ya mwaka huu ni Maadili, Haki za Binadamu, Utawala Bora na Mapambano dhidi yaRushwa ni jukumu la pamoja kati ya Serikali, Wananchi na wadau wengine.
Serikali ilianza kuadhimisha siku mbili Maadhimisho ya siku ya Maadili na haki za binadamu nchini , imetokana na siku mbili tofauti ambazo huadhimishwa kimataifa ambazo ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa pamoja na Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambapo kuanzia mwaka 2016 Serikali iliamua kuadhimisha siku hizi kwa pamojahivyo mwaka huu ni wa sita (6) kwa maadhimisho haya kufanyika kwa pamoja.
Taasisi Simamizi za Utawala Bora na Haki za Binadamu nchini zinazounganisha nguvu na kuhakikisha kuiwa maadhimisho hayo yanafanikiwa ni pamoja na: Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Katiba na Sheria,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretarieti ya Maadili ya Vingozi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.