KLABU MPYA 15 ZA MAADILI ZAANZISHWA WILAYANI MPWAPWA

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati, Dodoma imeanzisha klabu mpya 15 za Maadili kwa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Klabu hizo, zilizinduliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wlaya ya Mpwapwa Bi. Mwanahamisi Ally kati ya tarehe 22 hadi 25 Aprili, 2025 wakati wa zoezi maalum lililohusisha shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo.
Bi. Mwanahamisi ameipongeza Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa jitihada wanazofanya za kutoa elimu ya maadili kwa kada mbalimbali nchini.
‘’Kwa kweli niwapongeze katika hili maana mnafanya jambo ambalo lina manufaa makubwa kwa kizazi cha sasa na baadae kwa kutoa elimu ya maadili ambayo ni msingi kwa vijana hawa pamoja na Taifa zima,’’ alisema Bi. Mwanahamisi.
Shule za msingi zilizofanya uzinduzi wa klabu mpya ni; Tambi, Nana, Mwenzele, Mbori, Ikulu, Mlembule, Mpeta, Bumila, Kimaghai,Mapala, Manghangu na Vinghane, wakati shule za sekondari ni Mlembule, Kimaghai A na Kimaghai.
Akizungumza mara baada ya kufunguliwa kwa klabu ya Maadili shuleni kwake, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mlembule Bw. Stephano Mushi alishukuru Sekretarieti ya Maadili na uongozi wa Wilaya ya Mpwapwa kwa kuona umuhimu wa kuwa na klabu za Maadili na aliahidi kuisimamia vyema kwa kushirikiana na mwalimu mlezi.
‘’Tunashukuru kwa jambo hili, hii ni hatua kubwa kwetu na kutokana na changamoto za kimaadili zilizopo katika shule yetu, kuanzishwa kwa klabu kutawasaidia wanafunzi kujitambua na kuwa waadilifu na chachu katika kuleta mafanikio ya kitaaluma,’’alisema Mwalimu Mushi.
Kwa upande wake Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Joshua Mwambande alisema kuwa zoezi hilo ni endelevu kwa Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida na alisisitiza kuwa licha ya kufanikisha kuanzishwa kwa klabu hizo, Taasisi itafanya ziara za mara kwa mara kuangalia maendeleo ya klabu.
‘’Zoezi hili ni endelevu, tunaendelea kuanzisha klabu mpya na kuzihuisha klabu za zamani, tutazitembelea mara kwa mara kujua zipo katika hali gani,’’ alisisitiza Bw. Mwambande.