Jaji Mwangesi: Viongozi zingatieni Uadilifu

Jaji Mwangesi: Viongozi zingatieni Uadilifu
Viongozi wa Umma wametakiwa kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili waweze kuaminika na kukubalika katika jamii inayowazunguka.
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi ametoa wito huo Juni 14, 2021 jijini Arusha wakati akitoa mada kuhusu maadili kwa viongozi wa umma katika kikao cha Viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha.
Mhe. Mwangesi alisema kuwa, “Ni ukweli usiopingika kwamba viongozi waadilifu wanakubalika katika jamii na ni chachu kwa wananchi kuiga mifano ya uadilifu kutoka kwa viongozi wao.”
Kwa mujibu wa Jaji Mwangesi, kiongozi wa umma anapaswa kujipambanua kwa watu anaowaongoza kwa kutimiza wajibu wake bila kushurutishwa na kutumia uwezo na ushawishi alio nao kujenga uadilifu katika jamii.
Aidha Kamishna alisisitiza kuwa, kiongozi yeyote wa umma anapaswa kuwa na tabia na mwenendo usio kuwa na mashaka ili wananchi wamwamini na kuiamini Serikali anayoitumikia.
Katika hatua nyingine Jaji Mwangesi aliwakumbusha viongozi kuzingatia misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayomtaka kila Kiongozi kuzingatia Maadili katika utekelezaji wa majukumu yake, Kuepuka mwenendo unaohaibisha utumishi wa umma baada ya kuacha wadhifa husika; hususani kujiepusha na tabia za ulevi, uhuni, kujihusisha na biashara zisizohalali.
“Katika kuzingatia misingi hiyo viongozi wanalazimika kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na miongozo katika kutekeleza majukumu yao,”alisema.
Misingi ya maadili inayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uaminifu, huruma, umakini, kujizuia na tamaa na kuzingatia viwango vya juu vya maadili kadri iwezekanavyo. Misingi mingine ni kuzingatia haki, kutopendelea na kutenda kazi kwa uadilifu wa hali ya juu ili kulinda na kuimarisha imani ya wananchi na serikali.
“Jiepusheni na migongano ya kimaslahi kwani hairuhusiwi kufanya jambo au kutoa uamuzi kwa kuzingatia maslahi binafsi. Epukeni kuzingatia maslahi ya familia zenu au mtu mwingine yeyote mliye na uhusiano naye,” alisisitiza.
Awali akifungua kikaohicho, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela alisema kuwa ipo changamoto kwa baadhi ya Viongozi wa Umma kudhani kuwa maadili yanahusika na ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na madeni tu.
Mhe. Mongela alifafanua kuwa Viongozi wengi wanatimiza tu kipengele cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinachowataka kakujaza Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kila ifikapo mwisho wa mwaka, lakini mienendo yao sio mizuri na hairidhishi kwani baadhi ya viongozi ni walevi, watoro, watumiaji wa lugha isiyofaa, wezi wa mali za umma na tabia nyingine nyingi zinazoipa taswira mbaya dhana ya uongozi.
“Viongozi wa Umma tunatakiwa kuwa na madili mazuri yasiyotiliwa shaka na kuyaishi yale tunayopaswa kuzingatia kwani kiongozi yeyote katika ngazi au wadhifa wowote ni kioo cha jamii husika,” alisema.
Kikao hicho cha Kamishna wa Maadili na Viongozi wa Umma ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2021 ambapo Mhe. Mwangesi anatembelea wadau wa maadili, kutoa elimu na kusikiliza kero na malalamikoo yao kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.