ELIMU YA UJAZAJI TAMKO LA RASLIMALI NA MADENI KWA MTANDAO YATOLEWA RUVUMA.

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetoa mafunzo ya ujazaji na urejeshwaji wa Tamko la Raslimali na Madeni kwa njia ya Mtandao (Online Declaration System-DS) kwa Viongozi wa Umma wa mkoani Ruvuma pamoja na kuwakumbusha uzingatiaji wa masuala ya kimaadili wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yalifanyika ukumbi wa Bomba mbili tarehe 17 Desemba, 2024 mjini Songea na Viongozi wa Umma walioshiriki ni kutoka Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya, wakuu wa Taasisi zilizopo Ruvuma, Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma.
Akifungua mafunzo hayo, mgeni rasmi Katibu tawala Msaidizi (UTAWALA) Mkoa wa Ruvuma, Bw. Joel Mbewa aliwataka Viongozi wa Umma kujitahidi kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayolenga kuboresha utendaji kazi, kwani kwa sasa Serikali kila kitu kinakwenda kidigitali.
“Tumieni fursa hii kujifunza kwa bidii ili mfahamu vyema namna ya kutumia mfumo wa ODS kwani kama mnavyofahamu kuwa tarehe 31 ya mwezi Desemba ya kila mwaka, Viongozi wote tunatakiwa tuwe tumewasilisha Tamko la Rasilimali na Mdeni kwa Kamishna wa Maadili bila kuchelewa,” alisema Bw. Mbewa.
Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji wa Maadili, Bw. Salvatory Kilasara alisema lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo Viongozi wa Umma namna ya kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao kwani kwa sasa haipokei tena Tamko kutoka kwa kiongozi kwa njia ya nakala ngumu.
“kutokana na maendeleo ya Teknolojia Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma, imeturahisishia kazi ya kuwasilisha matamko hayo kwa kutumia mfumo wa ODS. Ni matumaini yangu kwamba kupitia mafunzo haya, kila mmoja wetu atanufaika na elimu hii ya ujazaji wa matamko haya kwa njia ya mtandao,” alisema Bw. Kilasara.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili Kanda ya Kusini, Bw. Filotheus Manula amewaambia Viongozi wa Umma kuwa Maadili kwa kiongozi wa Umma hayapimwi kwa kiongozi kuwa masikini au tajiri, kwani kiongozi anaweza kuwa masikini na akawa hana Maadili na kiongozi anaweza kuwa tajiri na akawa na Maadili.
Kiongozi wa umma ambaye atakuwa ametumikia utumishi wa Umma kwa zaidi ya miaka 10 lakini anakosa hata kumiliki kiwanja au nyumba au hana maendeleo yeyote, uyo kwetu tunamuona kama hana Maadili. Kwani Serikali inamlipa mshahara mzuri, anapata posho mbalimbali sasa anazipeleka wapi? Kwetu sisi hayo sio Maadili kwa Kiongozi wa Umma kwani tunahitaji Kiongozi wa Umma anayeleta maendeleo kwa wananchi na ya kwake Binafsi, alisema, Bw. Manula.
Afisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bi Ester Allamani amewatoa hofu viongozi kuhusu matumizi ya mfumo kuwa ni mfumo rahisi ambao kila Kiongozi anaweza kutumia bila changamoto yeyote kama akifuata taratibu na maelezo ya mfumo.