DIWANI WA KATA YA CHEYO AFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA MAADILI
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemfikisha Bw. Yusuph Khamis Kitumbo Diwani wa Kata ya Cheyo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za kushindwa kuwasilisha Tamko la Raslimali na Madeni kwa muda wa miaka minne mfulululizo.
Kikao hicho cha Baraza la Maadili kilifanyika tarehe 7 Juni, 2024 jijini Dodoma katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuongozwa na Mwenyekiti wake Jaji (Mst.) Rose Teemba pamoja na mjumbe wa Baraza hilo Bw. Peter Ilomo.
Wakili wa Serikali Bw. Hassan Mayunga ameliambia Baraza kuwa, “kitendo cha kiongozi huyo kushindwa kutoa Tamko la Raslimali na Madeni ni ukiukwaji wa kifungu cha 9(1)(b) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.”
Akitoa ushahidi mbele ya Baraza hilo kwa upande wa mlalamikaji Afisa Uchunguzi mwandamizi Bi. Halima Ramadhani Mnenge amesema hata baada ya kiongozi huyo kukumbushwa kwa njia ya barua kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya kumtaka atimize wajibu wa kisheria wa kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni, alishindwa kufanya hivyo.
Aidha, shahidi alieleza kuwa pamoja na kiongozi huyo kushindwa kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa muda wa miaka minne mfululizio tangu mwaka 2020, hata alipowasilisha Tamko lake, hakuzingatia muda uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
“Mwaka 2015 alipochaguliwa kuwa Diwani wa kata ya Cheyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, hakutoa Tamko ndani ya siku 30 kama Sheria ya Maadili inavyomtaka, badala yake alitoa tamko hilo mwaka 2016 baada ya kukumbushwa kwa barua. Mwaka 2017 pia hakutoa Tamko la Rasilimali na madeni kwa wakati,” aliliambia Baraza la Maadili.
Tangu mwaka 2020 hadi 2023, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haikupokea tamko lake la Rasilimali na Madeni.
Aidha, Diwani huyo katika utetezi wake aliliambia Baraza kuwa yeye hakuwa na Elimu yoyote kuhusu Ujazaji wa Matamko na hajawahi kupata mafunzo yoyote kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Tangu nilipochaguliwa kuwa diwani wa Kata ya Cheyo mwaka 2015, sijawahi kuhudhuria darasa lolote la masuala ya maadili.’
Hata hivyo amekiri kuchelewesha uwasilishaji wa Tamko la Rasillimali na Madeni la mwaka 2015 na mwaka 2016.
Alisema, “Tamko la mwaka 2015 na mwaka 2016 niliwasilisha kwa kuchelewa wakati matamko ya mwaka 2020 na 2021 niliyawasilisha kwa njia ya barua pepe.”
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mwenyekiti wa Baraza alimueleza mlalamikiwa kuwa, “tunashukuru, tumesikia utetezi wako Baraza litafanye uchunguzi na kutoa mapendekezo.”