DC MBOGWE NA DAS ARUSHA WATOA UTETEZI MBELE YA BARAZA LA MAADILI

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tarehe Machi 28, 2025 imewafikisha mbele ya Baraza la Maadili Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita Mhe. Sakina Jumanne Mohamed na aliyekua Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Jacob Julius Rombo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Kikao cha Baraza kimefanyika Makao Makuu ya Ofisi za Sekretarieti ya Maadili jijini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Rose Teemba.
Wakili wa Serikali Bi. Catherine Tibasana, aliliambia Baraza kuwa bila ya sababu za msingi Mhe. Sakina Mohamed wakati akitekeleza majukumu yake ya Ukuu wa wilaya ya Mbogwe, ameshindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na (c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Aidha, Wakili huyo wa Serikali alieleza kuwa Bw. Jacob Rombo (DAS) amekikuka matakwa ya kifungu cha 6(1)(j) na kifungu cha 12(1)(d) vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kanuni ya 3(2)(b) na (k) ya kanuni za udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.
Watuhumiwa wote wawili wamekana mashtaka hayo.
Shahidi wa mlalamikaji Bw. Innocent Shetui,alilieleza Baraza kuwa Mhe. Sakina wakati akitekeleza majukumu yake ameshindwa kufuata sheria na msingi ya maadili kwa kutumia nafasi yake kumshinikiza dereva kutoa ushahidi wa uongo kwa maafisa wa Sekretarieti ya Maadili wakati wa mahojiano, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
‘’Mhe. Sakina alimpigia simu dereva wake Bw. Origini Milinga akimtaka akiri kuwa alipokea fedha kutoka kwa Katibu Tawala Bw.Jacob Rombo wakati wakiwa msibani Kondoa, jambo ambalo sio kweli kwani dereva huyo hakupokea kiasi chochote cha fedha kutoka kwa DAS,” alilieleza Baraza na kuongeza kuwa “Mhe. Sakina alifanya hivyo huku akisisitiza kuwa kuna maafisa kutoka Sekretarieti ya Maadili watakupigia kukuuliza kama ulipata pesa kutoka kwa DAS.’’
Kwa upande wake Mhe. Sakina alikana tuhuma hizo na kumtaka shahidi alionyeshe Baraza vielelezo vinavyoonyesha mazungumzo hayo ya kumtaka Bw. Milinga kusema uongo kuhusu kupokea fedha hizo.
Shahidi wa pili wa mlalamikaji Bw Origini Milinga aliyewahi kumuendesha Mkuu huyo wa wilaya, alilieleza Baraza kuwa alisafiri pamoja na Mhe. Sakina kutoka Mbogwe kwenda Dodoma, lakini hakupokea pesa yoyote ya kujikimu wakati wa safari na kulazimika kulala ndani ya gari.
“Mhe. Mwenyekiti jukumu langu mimi nikiwa safarini na dereva ni kuhakikisha anakula na mimi nalipa hela, kama asinge kula, angekufa au angezimia safarini, tuhuma hizi dhidi yangu sio za kweli,” alieleza na kuongeza kuwa,” dereva anapodai sikumpa posho ya safari, sio jukumu langu mimi kama Mkuu wa wilaya.”
Bw. Milinga alilieleza Baraza kuwa walipofika Dodoma, Mkuu wa wilaya alimwambia ampeleke Kondoa kwenye msiba na walilala siku moja huko msibani bila kupewa posho yoyote.
Kwa hatua nyingine, Bw Jacob Rombo ambaye kwa sasa ni DAS wa wilaya ya Arusha wakati akitekeleza majukumu yake akiwa wilayani Mbogwe alishinikiza na kupokea shilingi 235,620/= kutoka kwa Bi. Helena Sekwa ambaye ni mhudumu wa kituo cha mafuta cha Mzingo Oil ili kujinufaisha kiuchumi jambo ambalo ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu na pia kinyume na mkataba kati ya ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbogwe na kampuni ya Mzingo Investment ambao ni wamiliki wa kituo hicho cha mafuta
Akimsomea shtaka lake, Wakili wa Serikali Bi. Tibasana alisema, ‘’Kitendo cha kuchukua pesa taslimu badala ya mafuta kama mkataba unavyosema ni ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.’’
Shahidi wa kwanza wa mlalamikaji Bw. Innocent Shetui aliliambia Baraza kuwa mnamo tarehe 26 Novemba, 2023 walinasa ‘clip’ ya sauti ya watu wawil kupitia anwani ya https://www.instagram.com/share/BAIxUVG9bS ambao ni Bw. Jacob Rombo (DAS) na Bi. Helena Sekwa (mhudumu wa kituo cha mafuta cha Mizingo Oil).
Alieleza kuwa, katika clip hiyo tulibaini kuwa Bw. Jacob alikua akishinikiza kupatiwa fedha badala ya mafuta na baada ya kufanya uchunguzi wa kina walibaini kuwa amekua akifanya hivyo kwa nyakati tofauti.
Bw. Jacob alipoulizwa kuhusu sauti inayosikika katika clip hiyo alikiri kuwa ni sauti yake.
“Ni kweli sauti ni ya kwangu nani kweli nilichukua 230,000/= badala ya mafuta kwa nia njema ili kiongozi wangu aliyekuwa safarini apate kutekeleza majukumu yake ya kazi,” alisema.
Shahidi wa tatu wa mlalamikaji Bi. Helena Sweka ambaye ni mhudumu wa kituo cha mafuta alikiri kuwa mnamo tarehe 19.11.2023 alimpatia DAS shilingi 235,620/= badala ya mafuta kiwango ambacho ni sawa na lita 100 za mafuta na tofauti na kibali cha kuombea mafuta.
“Kibali cha mafuta kilikuwa lita 150, nilijaza lita 50 kwenye gali na lita 100 nilitoa pesa kwasababu Bw. Jacob aliniambia ana dhalula anataka anataka pesa ya lita 100,” alisema.
Bwana Jacob aliliambia baraza kuwa, ‘’Ninaliomba Baraza lako tukufu liangalie dhamira yangu kwani siwezi kuchukua fedha hizo kwa matumizi yangu binafsi na kwamba imani ya Rais kwangu kama kijana itakua nimetenda kosa na nimemuangusha Mhe. Rais kama nitakutwa na hatia hizo,’’alisema Bw. Jacob.