Uwasilishaji wa Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inapenda kuwakumbusha viongozi wote wa umma walioainishwa kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Sura ya 398), kuwa upokeaji wa Tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni kwa mwaka 2023, umeanza tangu tarehe 01 Oktoba, 2023 na utamalizika tarehe 31 Desemba, 2023.
Uwasilishaji wa Tamko hilo kwa Kamishna wa Maadili ni kwa mujibu wa kifungu cha 9(1)(b) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kwamba kutoa Tamko la uongo, potofu, kuchelewa ama kushindwa kuwasilisha Tamko hilo kwa kipindi kilichoainishwa ni ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria tajwa.
Kiongozi anatakiwa kupakua fomu katika tovuti ya Taasisi yenye anwani www.maadili.go.tz na kuijaza kisha kuwasilisha Tamko husika kwa kufika moja kwa moja katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu zilizoko Jengo la PSSSF Kambarage, Mtaa wa Jakaya Kikwete - Dodoma, Ofisi za Kanda ya Kati zilizoko Viwanja vya Nanenane – Dodoma, Ofisi za Kanda Maalum Dar es Salaam zilizoko Barabara ya Ohio karibu na Benki ya CRDB Holland House, Dar es Salaam, Ofisi za Kanda ya Kaskazini zilizoko katika Jengo la Hazina – Arusha, Ofisi za Kanda ya Ziwa zilizoko Jengo la NSSF, Mtaa wa Kenyatta - Mwanza, Ofisi za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zilizoko Jengo la NHIF – Mbeya, Ofisi za Kanda ya Mashariki zilizoko Jengo la NSSF – Morogoro, Ofisi za Kanda ya Magharibi zilizoko Mkabala na Hoteli ya Orion – Tabora na Ofisi za Kanda ya Kusini zilizoko Jengo la Maadili – Mtwara, Mtaa wa Chikongola Barabara ya TANU. Aidha, kiongozi anaweza pia kuwasilisha Tamko kwa njia ya posta kupitia “registered mail” ikiwemo “ems.”
Viongozi wanakumbushwa kuwa Tamko linalopokelewa ni nakala halisi (Original Copy) na sio lililorudufiwa (Photocopy) au lililokuwa “scanned” na kutumwa kwa njia ya baruapepe.